Home Habari za michezo KOCHA YANGA YAKIRI MAKOSA, AONA SOMO DODOMA JIJI

KOCHA YANGA YAKIRI MAKOSA, AONA SOMO DODOMA JIJI

58
0

KOCHA msaidizi wa Yanga SC, Patrick Mabedi, ameweka wazi tathmini yake baada ya kikosi hicho kumaliza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC, amesema bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho licha ya timu yake kuonyesha kiwango kizuri uwanjani.

Akizungumza baada ya mechi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Mabedi amekiri  kuwa Yanga iliruhusu kufungwa bao ambalo halikupaswa kutokea, akieleza kuwa lilitokana na makosa ya kimchezo ambayo yalipaswa kuzuiwa mapema.

Kocha huyo alisema makosa hayo ni sehemu ya mchezo wa soka, lakini amesisitiza kuwa ni lazima yafanyiwe kazi kwa kina ili kuepuka kuathiri matokeo ya michezo ijayo, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani ni mkubwa.

Mabedi ameeleza kuwa ratiba ngumu imekuwa changamoto kwa kikosi chake, hususan kutokana na safari za kimataifa walizofanya hivi karibuni, hali iliyopunguza muda wa maandalizi kabla ya kuikabili Dodoma Jiji.

“Muda mfupi wa maandalizi baada ya kurejea kutoka nje ya nchi uliathiri maandalizi ya timu, lakini pamoja na hilo, tunaridhishwa na namna wachezaji walivyopambana uwanjani licha ya uchovu,” amesema Mabedi.

Ameongeza  kuwa wachezaji walionyesha nidhamu, morali na dhamira ya kupambana hadi dakika ya mwisho, huku benchi la ufundi likiendelea kufanya kazi ya kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza ili kuboresha zaidi kiwango cha timu kadri msimu unavyoendelea.

Kocha huyo msaidizi pia amewashikuru  mashabiki wa Yanga kwa sapoti kubwa wanayoendelea kutoa, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu katika kuipa timu nguvu ya kupambana katika kila mchezo, iwe ni nyumbani au ugenini