BAADA ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuufungia Uwanja wa KMC Complex, hatma ya Yanga SC kucheza mechi zake za nyumbani sasa ipo mikononi mwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kwa sasa ni mapema kuweka wazi ni uwanja gani watakaoutumia kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wakisubiri maelekezo rasmi kutoka Halmashauri husika.
Kamwe amesema Yanga tayari imepokea taarifa ya kufungiwa kwa Uwanja wa KMC Complex pamoja na sababu zilizopelekea hatua hiyo, kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya klabu na Halmashauri, ambayo imewataka wawe na subira.
“Hadi sasa hatuna mechi za ligi, ratiba inaanza tena Februari 14 au 15. Kwa sasa tunajiandaa na mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa baada ya mchezo wa nyumbani dhidi ya JS Kabylie utakaochezwa Februari 13, wanatarajia kupokea taarifa rasmi kutoka Halmashauri kuhusu hatua ya mwisho ya ukamilishaji wa uwanja huo.
“Endapo uwanja hautakuwa umekamilika, tutalazimika kuangalia mbadala wa uwanja wa nyumbani, iwe ni Sumbawanga au hata kutumia uwanja wa watani zetu, Meja General Isamuhyo,” amesema Kamwe.