Home Habari za michezo YANGA KUSAKA POINT TATU ZA AL AHLY

YANGA KUSAKA POINT TATU ZA AL AHLY

30
0

KIKOSI cha Yanga SC kesho kinashuka dimbani kikitupa karata yake muhimu katika harakati za kusaka alama tatu, wakati kitakapowaalika Al Ahly ya Misri kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo utachezwa Jumamosi Januari 31 katika dimba la New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, ambapo Yanga itakuwa mwenyeji ikihitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na dhamira ya kufuta kumbukumbu mbaya ya kipigo cha mabao 2-0 ilichokipata ugenini dhidi ya Al Ahly kwenye uwanja wa Borg El Arab, jijini Alexandria nchini Misri, matokeo ambayo yaliifanya kazi yao katika kundi kuwa ngumu zaidi.

Huo ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga kupoteza katika hatua ya makundi, baada ya awali kuanza kwa kishindo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS FAR katika uwanja wa nyumbani, pamoja na kupata sare ugenini dhidi ya JS Kabylie.

Kwa kutambua umuhimu wa mchezo huo, Yanga inatarajiwa kushuka uwanjani kwa tahadhari kubwa, nidhamu ya hali ya juu na sapoti kubwa ya mashabiki wao, wakiamini ushindi nyumbani unaweza kufufua matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo.

Macho yote sasa yanaelekezwa Zanzibar, ambapo Yanga itahitaji kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani ili kuandika historia mpya dhidi ya wababe hao wa soka barani Afrika.