BAADA ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri, beki wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, amesema matokeo hayo yamewaongezea hasira chanya ya kwenda kusaka ushindi katika mchezo ujao dhidi ya FAR Rabat utakaochezwa nchini Morocco.
Tshabalala amesema lengo lao kubwa katika mchezo huo lilikuwa ni kupata pointi tatu wakiwa nyumbani, lakini hawakufanikiwa kutimiza dhamira hiyo na badala yake wakaambulia pointi moja baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa hao wa Afrika.
Hata hivyo, beki huyo ameeleza kuwa matokeo hayo si mabaya kwa kuzingatia ubora, uzoefu na ugumu wa Al Ahly, akisisitiza kuwa Yanga walipambana kwa nguvu kubwa na kuonyesha ushindani wa hali ya juu katika mchezo mzima.
Ameongeza kuwa kwa sasa kikosi cha Yanga kimeanza kujipanga vizuri kuelekea mechi mbili zilizosalia katika hatua ya makundi, akisema maandalizi yatafanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya yatakayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kwa mujibu wa msimamo wa Kundi B, Al Ahly wanaongoza wakiwa na pointi nane, wakifuatiwa na Yanga wenye pointi tano, huku FAR Rabat wakiwa na pointi tano pia na JS Kabylie wakishika mkia kwa pointi mbili, hali inayoonyesha ushindani mkali katika kundi hilo.
“Kundi bado lipo wazi, tunaenda kupambana kusaka ushindi ili kusonga mbele na tuna nafasi. Tunaenda Morocco kupambana kusaka ushindi,” amesema Tshabalala, huku Yanga wakitarajiwa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya FAR Rabat Februari 7 nchini Morocco.