WINGA mpya wa Yanga, Buba Jammeh, anatarajiwa kujiunga na wachezaji wenzake nchini Morocco mara baada ya timu hiyo kuwasili kwa ajili ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat.
Kikosi cha Yanga kinasafiri leo Jumanne, Februari 03, 2026, mchana kuelekea Morocco kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo ya marudiano, huku Jammeh akipangwa kuungana na timu hiyo akiwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, nyota huyo ataungana na kikosi moja kwa moja Morocco, ambapo timu itakuwa imewasili kwa ajili ya mchezo huo mzito wa kimataifa.
Kamwe amesema msafara wa Yanga unajumuisha wachezaji 23 pamoja na benchi la ufundi, ambapo leo watapumzika Dubai kabla ya kuendelea na safari kuelekea Morocco kesho.
“Wachezaji 22 wataondoka hapa nchini, huku Buba Jammeh akijiunga na kikosi nchini Morocco. Kwa ujumla, msafara utakuwa na watu 50 wakiwemo viongozi na mashabiki wanaokwenda kuisapoti timu,” amesema Kamwe.
Ameeleza kuwa kikosi kilichochaguliwa na Kocha Mkuu, Pedro Goncalves, kiko salama bila majeruhi wowote, jambo linaloongeza matumaini kuelekea mchezo huo mgumu wa ugenini.
Yanga itashuka dimbani Februari 7, 2026, kucheza dhidi ya AS FAR Rabat katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikilenga kusaka matokeo chanya yatakayoiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.