MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu na kutumia hasira walizonazo kama chachu ya kuijenga Simba, badala ya kuzigeuza kuwa chanzo cha kuvunja umoja na mshikamano wa klabu.
Akizungumza kufuatia mwenendo usioridhisha wa Simba katika michuano ya kimataifa msimu huu, Ahmed amesema anaelewa maumivu na hasira za mashabiki, lakini amesisitiza kuwa hali hiyo isiwapelekee kupoteza misingi ya utu, heshima na mshikamano wao.
“Mashabiki wenzangu wa Simba, najua tuna hasira kufuatia mwenendo wetu kwenye michuano ya Afrika msimu huu. Hata hivyo, hasira hizo zisifanye tuvunje misingi yetu ya utu na heshima kwa viongozi wetu na sisi wenyewe,” ameandika Ahmed.
Ameongeza kuwa Simba haina budi kukubali kuwa msimu huu haukuwa mzuri kimataifa, akisisitiza kuwa hali hiyo hutokea kwa timu nyingi duniani, hivyo haipaswi kuwa chanzo cha lawama zisizo na mwisho wala migawanyiko.
“Tusipoteze muda kufarakana, kubagazana mitandaoni au kupitia vyombo vya habari. Tukumbuke kuwa wanaotuchukia hunufaika zaidi na marumbano yetu na hujitahidi kuchochea tuvurugane,” ameandika.
Ahmed amesema kwa sasa Simba inapaswa kuelekeza nguvu, akili na maarifa katika mashindano ya ndani ambayo bado yana matumaini, akitaja Ligi Kuu ya NBC na Kombe la CRDB kuwa ndiyo fursa muhimu zilizobaki msimu huu.
“Badala ya kucharurana na kupoteza mwelekeo, ni vyema tukawekeza nguvu zetu huko ili tupate mafanikio,” amesema.
Ahmed amewataka mashabiki kutovunjika moyo, akisisitiza umuhimu wa kumaliza msimu kwa heshima na kuanza maandalizi ya kurejea kwa nguvu zaidi msimu ujao wa mashindano ya kimataifa.
“Tusivunjike moyo ndugu zangu wa Simba, tujipange kwenye ligi za ndani na tujipange kurejea kwa kishindo msimu ujao kimataifa. Pia mechi zilizobaki tusimalize kinyonge,” amesema.