Home Habari za michezo YANGA KUFUATA TIKETI YA ROBO FAINALI MOROCCO

YANGA KUFUATA TIKETI YA ROBO FAINALI MOROCCO

0

OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, ameweka wazi malengo ya kikosi hicho kuelekea mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat, kuondoka na alama tatu au angalau pointi moja ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Februari 7 nchini Morocco, katika mchezo wa ugenini dhidi ya wenyeji AS FAR Rabat, ambao una umuhimu mkubwa kwa hatma ya kundi lao katika michuano hiyo ya kimataifa.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu, Kamwe amesema kocha mkuu Pedro Goncalves tayari amewaweka sawa wachezaji kisaikolojia baada ya mechi ngumu dhidi ya Al Ahly, akisisitiza kuwa sasa nguvu zote zimeelekezwa kwenye pambano dhidi ya AS FAR.

“Sasa tunaelekea kwenye mechi muhimu dhidi ya AS FAR Rabat. Tuna kila sababu ya kwenda kupambana kutafuta ushindi, na kama haitapatikana basi angalau tupate sare,” amesema Kamwe.

Ameongeza kuwa matokeo yoyote chanya yatakuwa na mchango mkubwa kwa Yanga katika safari yao ya kufuzu, huku ushindi ukiwa ni tiketi muhimu ya kujihakikishia nafasi ya robo fainali wakiwa ugenini.

Kamwe  amesema mchezo huo utafanyika bila uwepo wa mashabiki, jambo analoamini linaweza kuwapa nafasi Yanga kupambana bila presha ya nje. “Itakuwa mechi ya wachezaji pekee. Hilo ni jambo zuri kwetu kupambana kwa nguvu zote na kutafuta matokeo mazuri ugenini,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Kamwe, kocha Pedro amewataka wachezaji kuingia uwanjani wakiwa na mawazo ya ushindi pekee, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya kufikiria kupoteza katika mchezo huo mgumu wa ugenini.