KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves, amesema uzoefu walioupata katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakuwa chachu ya maboresho makubwa, amesisitiza kuwa timu hiyo itarejea ikiwa na ushindani mkubwa zaidi katika anga la kimataifa.
Pedro amesema kikosi chake kilicheza kwa nguvu, akili, na mipango madhubuti kuhakikisha kinapata matokeo chanya.
“Wachezaji wamefanya kazi kubwa kutafuta matokeo kwenye mchezo wetu wa mwisho na walionyesha hilo uwanjani. Kwa kila namna ninawapongeza kwa sababu walipambana kwa moyo wote na walifuata maelekezo kwa umakini,” amesema.
Kocha amesema kuwa ushindi walioupata ni matokeo ya juhudi, nidhamu, na mshikamano wa wachezaji ambao hawakukata tamaa licha ya presha kubwa ya kusaka tiketi ya kusonga mbele.
Ameongeza kuwa Uzoefu huu, umewasaidia wachezaji kujifunza mengi kuhusu mashindano ya kimataifa, hatua ambazo zitakuwa muhimu kwa maandalizi ya msimu ujao.
“Tumepata somo kubwa kutoka kwenye ushindani wa hatua ya makundi. Sasa nguvu zote zitaelekezwa katika kujijenga upya, kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha Yanga inarejea ikiwa imara zaidi katika mashindano ya kimataifa,” amesema Pedro.
Yanga ilimaliza michuano hiyo kwa kishindo licha ya kuaga mapema. Februari 15, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, timu hiyo ilitoka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya JS Kabylie, lakini ushindi huo haukutosha kuwavusha hatua ya robo fainali.
Baada ya michezo ya Kundi B kumalizika, Yanga ilishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane, huku nafasi mbili za juu zikichukuliwa na Al Ahly SC na AS FAR Rabat, ambazo ndizo zilizofanikiwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Pedro amesema timu ina malengo makubwa, na msimu ujao watarudi wakiwa na nguvu zaidi, ushindani mkali, na ndoto ya kufanikisha matokeo makubwa kimataifa.