KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameanza kutekeleza mkakati maalum wa kuhakikisha timu yake inapata ushindi mapema kwa kufunga angalau mabao mawili ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Mkakati huo umeanza kuonekana katika michezo ya hivi karibuni, hususan kwenye Kombe la CRDB Bank Federation Cup ambapo Simba iliichapa Greenland kwa mabao 3-0.
Katika mchezo huo, mabao mawili yalipatikana kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza la tatu kipindi cha pili, ishara ya dhamira ya kumaliza kazi mapema.
Mbinu hiyo pia ilijirudia katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons, ambapo Simba ilishinda mabao 2-0 huku mabao yote yakifungwa ndani ya kipindi cha kwanza.
Hali hiyo imeonyesha wazi msisitizo wa kocha huyo katika kuutawala mchezo mapema na kupunguza presha ya baadaye.
Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, benchi la ufundi limeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha timu inatumia vyema dakika 45 za mwanzo.
Amesema lengo ni kuingia mapumziko wakiwa na faida ya mabao itakayowapa utulivu na kujiamini kipindi cha pili.
Ahmed ameeleza kuwa Barker ameandaa “dozi” maalum kwa wapinzani wao, akiamini presha ya mapema itawavuruga na kuipa Simba nafasi ya kutawala mchezo kwa uhuru zaidi.
Ameongeza kuwa maandalizi yamejikita katika kuongeza kasi ya mchezo, umakini mkubwa na matumizi sahihi ya nafasi za kufunga.
“Mipango ya kocha ni kumaliza mchezo kipindi cha kwanza. Tunahitaji mabao mengi mapema ili kudhibiti mchezo na kupunguza presha baadaye,” amesisitiza Ahmed.
Mkakati huo unaongeza presha kwa wapinzani wao kuelekea Kariakoo Derby dhidi ya Yanga SC, utakaopigwa Machi Mosi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.