BAADA ya kupata sare tatu mfululizo, uongozi wa klabu ya Yanga umechukua hatua ya kuimarisha benchi la ufundi kwa kuthibitisha rasmi kurejea kwa Abdihamid Moalin ndani ya kikosi hicho, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kurekebisha mwenendo wa timu.
Moalin anarejea katika nafasi ya kocha msaidizi, ambapo atafanya kazi kwa karibu na Kocha Mkuu, Pedro Gonçalves, ambaye anaendelea kuiongoza timu hiyo katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Hatua hiyo inakuja katika kipindi ambacho Yanga inahitaji utulivu na uzoefu wa kiufundi, hasa wakati ushindani wa ligi na michuano mingine ukiwa umeongezeka kwa kasi.
Moalin si mgeni ndani ya Yanga, kwani aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na kocha msaidizi chini ya makocha waliopita, akiwemo Sead Ramović na Miloud Hamdi.
Uzoefu wake mkubwa ndani ya klabu hiyo unampa nafasi ya kuelewa vyema mazingira ya timu, wachezaji na matarajio ya mashabiki, jambo linalotarajiwa kumwezesha kuanza kutoa mchango mara moja.
Uongozi wa Yanga unaamini kurejea kwake kutaongeza nguvu katika benchi la ufundi na kusaidia timu kufikia malengo yake, ikiwemo kutwaa mataji na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Maamuzi hayo ni baada ya timu hiyo kutoka sare katika michezo mitatu mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kuchukua hatua ya kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi.