Home Habari za michezo KIPIGO CHA SIMBA CHAZUA WITO WA UMOJA NDANI YA YANGA

KIPIGO CHA SIMBA CHAZUA WITO WA UMOJA NDANI YA YANGA

0

MSEMAJI wa Yanga SC, Ali Kamwe, amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu na kuendelea kuiunga mkono timu yao licha ya matokeo ya hivi karibuni kwenye michezo ya fainali ya Muungano dhidi ya Simba .

Yanga imeshindwa kutetea taji lao la Ubingwa wa Muungano baada y kukubali kichapo cha bO 1-0 dhidi ya Simba uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.

Kamwe ameweka wazi kuwa katika soka kuna nyakati za furaha na changamoto, hivyo ni muhimu kwa Wananchi kubaki wamoja na kuamini katika mchakato wa timu yao.

Amesema kuwa mechi za dabi zimekuwa na ushindani mkubwa, huku wapinzani wao wakionyesha kiwango kizuri, lakini hilo halipaswi kuwakatisha tamaa mashabiki wa Yanga.

Badala yake, Kamwe amesisitiza kuwa ni wakati wa kusimama pamoja na kuipa timu nguvu zaidi, akiamini kuwa matokeo bora yatarejea kadri muda unavyokwenda.

Kamwe ameongeza kuwa licha ya maumivu ya kupoteza mechi muhimu, bado kuna malengo makubwa mbele yao, hususan katika Ligi Kuu.

Amebainisha kuwa kikosi kina uwezo wa kupambana na kurejesha heshima ya timu hiyo, ikiwa kila mmoja atabaki na imani na kujitoa kwa dhati.

Amekiri kuwa hali ya uchovu, hasira na huzuni inaweza kuwapo kwa mashabiki na wachezaji kwa wakati mmoja, lakini ameeleza kuwa hali hizo ndizo zinazojenga timu imara na mabingwa wa kweli

“Nyakati ngumu hujenga uimara na uzoefu unaohitajika kufikia mafanikio makubwa. benchi la ufundi pamoja na wachezaji watarejea mazoezini ili kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita,” amesema Kamwe.

Ameeleza kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha wanarejea wakiwa bora zaidi na tayari kwa changamoto zijazo huku amewapongeza  mashabiki wa Yanga kwa sapoti yao isiyoyumba na kuwaahidi kuwa timu haitowaangusha.

. Amehimiza kuendelea kuwa pamoja, akisisitiza kuwa Yanga ni kubwa kuliko matokeo ya mechi moja, na ushindi utaendelea kuwa sehemu ya safari yao.