Habari za michezo
SIMBA YATIKISWA NA KAULI YA ZIMBWE JR, MBIO ZA UBINGWA ZAZIDI KUPAMBANA MOTO
Vardo
May 22, 2026
10:48 am
BAADA ya kukaa nje kwa muda kutokana na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja, beki wa kushoto wa Yanga SC, Mohammed Hussein (Zimbwe JR), amesisitiza kuwa sasa Wananchi wamekuwa “hatari zaidi” katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Zimbwe JR alilazimika kukosa michezo kadhaa mwezi Mei kutokana na majeraha, hali iliyowapa presha Yanga SC katika kipindi ambacho ushindani wa ubingwa ulikuwa ukizidi kupamba moto
Kutokuwepo kwake kulionekana kama pengo muhimu, hasa kwenye safu ya ulinzi ya pembeni.
Hata hivyo, beki huyo sasa amerudi kikosini akiwa fiti na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani leo dhidi ya Singida BS katika mchezo utakaopigwa kwenye KMC Complex.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake, hasa ikizingatiwa kuwa presha ya mbio za kileleni imeongezeka kila uchao kadri msimu unavyokaribia ukingoni.
Akizungumzia hali ya ushindani wa ligi, Zimbwe JR amesema tofauti ya pointi kati ya Yanga na wapinzani wao Simba SC imepungua kutoka alama tano hadi mbili, hali anayoiona kama onyo kubwa kwa timu yake.
“Tulikuwa mbele kwa tofauti ya alama tano, sasa zimebaki mbili tu. Hii ni tahadhari kubwa kwetu. Inatufanya tujikite zaidi kwenye kila mchezo na kuhakikisha hatufanyi makosa tena,” amesema.
Ameongeza kuwa katika hatua hii ya msimu, kila mchezo umebeba uzito wa fainali, na hakuna tena nafasi ya kupoteza hata pointi moja.
“Alama tatu sasa ni muhimu sana. Hatuna nafasi ya kuruhusu makosa. Tunahitaji umakini wa hali ya juu ili tufikie malengo yetu ya kutetea ubingwa,” ameongeza.
Pia ametoa wito kwa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi uwanjani kuisapoti timu yao, akisisitiza kuwa nguvu yao ni silaha muhimu katika kipindi hiki kigumu cha ushindani.
“Mashabiki wetu ni sehemu ya kikosi. Tunawahitaji sana kipindi hiki. Tukishikamana pamoja, tunaweza kufanikisha malengo yetu,” amesema.
Wakati mbio za ubingwa zikiendelea kushika kasi, Yanga SC sasa inalazimika kucheza kwa umakini wa hali ya juu katika kila dakika, huku kila kosa dogo likiweza kubadilisha hatima ya msimu mzima wa ligi.