Uchungu Wa Marry Mjema: Ailalamikia Geita Gold Queens Kwa Kutomlipa Sh1.75M Ya TFF
Mchezaji wa Geita Gold Queens, Marry Mjema, amefunguka kueleza masikitiko yake baada ya klabu hiyo kushindwa kumpa mshahara wake wa Sh1.75 milioni, licha ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa amri ya kulipwa fedha hizo tangu mwezi Mei mwaka huu.
Akizungumza na Soka la Bongo, Marry alieleza kuwa changamoto zake zilianza rasmi mwaka 2023 wakati wa mchezo wa robo fainali wa Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Masala Princess katika Uwanja wa Nyamagana.
Kwenye mchezo huo, alipata jeraha baya la goti mnamo dakika ya 86 baada ya kugongwa kwa nyuma. Licha ya maumivu makali, aliendelea kupambana na timu hiyo mpaka ikafanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL).
Kutoka Hospitali HADI Kwa Waganga Wa Asili
Baada ya timu kufanikiwa kupanda Ligi Kuu na kuanza maandalizi ya msimu wa 2023/24, Marry anadai kuwa hakupata matibabu sahihi ya kibingwa aliyoyatarajia. Badala ya kupelekwa hospitalini kwa ajili ya vipimo na matibabu ya kina, alipelekwa kwa waganga wa asili.
Ugumu wa maisha na majeraha uliambatana na msiba mzito kwenye familia yake:
“Mimi ndiyo baba na mama kwenye familia. Niliwaomba mshahara nikamtibie baba yangu aliyekuwa anaumwa sana Moshi, lakini wakakataa. Baba yangu alifariki nikiwa sina hata senti moja ya kumsaidia,” alieleza Marry kwa uchungu.
Mgogoro Wa Mkataba Na Uamuzi Wa TFF
Mbali na matibabu, kulizuka mgogoro mwingine kuhusu mkataba wake. Marry anaeleza alisaini mkataba wa miaka miwili, lakini baadaye klabu ikawasilisha mkataba wa miezi tisa pekee.
Suala hilo lilipelekwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF. Kupitia barua rasmi yenye kumbukumbu TFF/ADM/DLM.163.2026 ya Mei 10, 2026, kamati hiyo ilisikiliza shauri hilo.
Kamati ilibaini kuwa mchezaji huyo alikuwa anadai mishahara ya miezi saba (7), ambapo kila mwezi alipaswa kulipwa Sh250,000. TFF iliiamuru klabu ya Geita Gold Queens kumlipa Marry Mjema jumla ya Sh1,750,000.
Ndoto Za Soka Zikididimia
Hadi sasa, Marry hajapokea hata stahiki hizo huku akipitia maumivu makali ya kiafya. Tayari amefanyiwa upasuaji mara tatu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa msaada wa Jeshi, lakini bado hawezi kukimbia na mguu wake huvimba anapofanya kazi nzito.
Kutokana na hali hiyo, ndoto zake za kuendelea kucheza soka zimefifia na sasa anoomba kupata mtaji wa biashara ili kuanza maisha mpya nje ya uwanja.
Kauli Ya Geita Gold Queens
Alipotafutwa Meneja wa Geita Gold Queens, Sabina Mkama, alisema anafahamu uwepo wa kesi hiyo lakini hakuwa tayari kutoa maelezo ya moja kwa moja:
“Yeye Marry anajua sitakuwa na majibu ya moja kwa moja, japokuwa kesi naijua. Anajua nani wa kuwasiliana naye… mimi ni mshikaji wake sana, sijafuatilia waliishiaje,” alisema Sabina.
Jitihada za kumtafuta Ofisa Mtendaji Mkuu wa Geita Gold Queens, Paulo Ojina, pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Hadhi za Wachezaji wa TFF, Evans Mgeusa, hazikufanikiwa kwani simu zao hazikupokelewa hadi habari hii inawekwa hewani.