Coastal Union Yainasa Saini ya Ahmed Issa Mbele ya Simba SC
Klabu ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ imefanikiwa kuimarisha safu yake ya ulinzi baada ya kunasa saini ya aliyekuwa kipa namba moja wa timu ya JKU, Ahmed Issa, kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu wa 2026/2027.
Kabla ya kumwaga wino Coastal Union, kipa huyo alikuwa kwenye rada za Simba SC ambapo alifikia hadi kambini kwa takribani siku tatu. Hata hivyo, mpango wa kujiunga na Wekundu wa Msimbazi ulikwama dakika za mwisho kutokana na viongozi wa Simba kushindwa kufikia makubaliano na klabu ya JKU, ambayo ilikuwa na mkataba wa miaka miwili na Issa.
Coastal Union ilitumia vyema fursa hiyo kwa kuingia kwenye mazungumzo na JKU na kufanikisha biashara hiyo haraka.
Akizungumzia usajili huo, Ahmed Issa alithibitisha kujiunga na Coastal Union akisema:
“Mimi kwa sasa ni mchezaji halali wa Coastal Union. Nimeshasaini mkataba na nipo kambini nikiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi zijazo.”
Kipa huyo aliongeza kuwa kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa ndoto yake ya muda mrefu, ndiyo maana aliamua kuvumilia na kubaki JKU licha ya ofa kadhaa kutoka timu za Zanzibar.
Katika msimu wa 2025/2026 wa Ligi Kuu Zanzibar, Ahmed Issa alimaliza akiwa kipa wa pili kwa kuwa na michezo mingi bila kuruhusu bao (clean sheets 10), nyuma ya Hamad Ubwa wa Mlandege (clean sheets 12). Pia, Issa alitwaa tuzo ya Kipa Bora wa Kombe la Muungano 2025 lililofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba.