Ali Kamwe Afichua Sababu Gomez, Aziz Ki Kuchelewa Yanga SC
OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amefichua kinachoendelea kwa nyota wawili wanaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa klabu hiyo, Selemani Mwalimu ‘Gomez’ na Stephane Aziz Ki, akibainisha kuwa kwa sasa wanaendelea ‘kupikwa’ kikamilifu na Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi.
Wachezaji hao wawili bado hawajapata nafasi ya kuanza kwenye michezo rasmi ya Yanga, hali ambayo imezua shauku kubwa kwa mashabiki wanaotamani kuona mchango wao uwanjani kulingana na ukubwa wa usajili wao.
Akifafanua hali hiyo, Kamwe ameeleza kuwa kuchelewa kwao kujiunga na kambi kulifanya wahitaji muda zaidi wa kuzoea mazingira, mfumo pamoja na mbinu za kocha, hivyo benchi la ufundi limeamua kutowaharakisha uwanjani kabla hawajawa tayari.
“Wachezaji hao bado wanaendelea kupikwa na kocha Manqoba katika uwanja wa mazoezi. Pindi watakapokuwa tayari na kwenda sawa na kasi pamoja na mbinu za timu, wataanza kutumika kwenye michezo ya Ligi Kuu na mashindano mengine,” alisema Kamwe.
Ameongeza kuwa nyota hao wanaendelea na programu maalum katika kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town, Kigamboni, huku benchi la ufundi likifuatilia kwa karibu maendeleo yao kabla ya kuwapa nafasi uwanjani.
“Kuna mechi nyingi mbele yetu, tusiwe na haraka. Kocha akijiridhisha kuwa kile anachokitaka kimefikiwa, basi mashabiki wataanza kuwaona uwanjani,” aliongeza.
Gomez alijiunga na Yanga akitokea kwa watani zao Simba SC katika usajili uliovuta hisia za wengi, wakati Aziz Ki akirejea klabuni hapo akiwa na mategemeo makubwa kama ‘X-Factor’ ya kikosi hicho. Kwa sasa, macho ya mashabiki wa Yanga yanasubiri kuona ni lini Mngqithi atawapa nafasi nyota hao kuanza mapambano.