“Dabi Haina Friendship, Ni Do or Die!” – Simba Yaweka Wazi Mipango Yote Dhidi ya Yanga
MENEJA wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini imeipa timu hiyo sehemu kubwa ya maandalizi iliyokuwa imeilenga, huku akisisitiza kuwa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga si mchezo wa urafiki, bali ni vita ya kutafuta matokeo.
Rweyemamu amesema kambi hiyo ilikuwa mwendelezo wa maandalizi ya awali yaliyofanyika Rwanda, ambako Simba pia ilishiriki mashindano ya Kagame, kabla ya mapumziko ya FIFA kutumiwa kurekebisha mapungufu yaliyoonekana katika maandalizi ya msimu.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tumefika salama. Tumetumia takribani siku 10 kwa ajili ya maandalizi baada ya mapumziko ya kalenda ya Fifa. Tumecheza mechi tatu na baada ya hapo tunaingia kwenye Champions League, mechi za mtoano ambazo tunatarajia zitatupeleka hatua ya makundi, Mwenyezi Mungu akijalia,” amesema.
RWYEMAMU: TUMETENGENEZA MAPUNGUFU
Akieleza umuhimu wa kambi hiyo, Rweyemamu amesema Simba ililazimika kutumia nafasi hiyo kuendeleza kazi iliyoanza Rwanda, huku mapumziko ya FIFA yakitoa muda wa kurekebisha maeneo ambayo timu haikufanya vizuri.
“Ilikuwa ni kambi ndogo ya kuendeleza ile ya pre-season tuliyofanya Rwanda, ambayo tulishirikisha pia mashindano ya Kagame. Tulipata siku chache kule, hivyo tukaona FIFA Break inaweza kutusaidia kurekebisha mapungufu ambayo tulishia nayo,” amesema.
“DABI HAINA FRIENDSHIP”
Akizungumzia Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, Rweyemamu amesema Simba haitaki kubebwa na historia ya matokeo ya nyuma, licha ya kukiri kuwa wapinzani wao wamekuwa na matokeo mazuri katika baadhi ya mechi za hivi karibuni.
“Katika soka hakuna kuwa mnyonge, lakini pia tusiende na historia. Ni kweli katika mechi kama tatu au nne hatujafanya vizuri zaidi ya Yanga, lakini kama mnakumbuka msimu uliopita tulipata pointi kwenye ligi na tuliweza pia kushinda,” amesema.
Akaongeza: “Mechi ya Simba na Yanga haina friendship, haina ligi, mwisho wa siku ni mechi ya ‘do or die’.”
SIKU 5–6 ZA MOTO
Rweyemamu amesema Simba bado ina siku kadhaa za kuendelea kukinoa kikosi kabla ya kukutana na Yanga, akisisitiza umuhimu wa kutumia muda huo kuboresha zaidi maandalizi.
“Maandalizi ya kule yalikuwa miongoni mwa maandalizi ya mechi ya Young Africans, lakini mwisho wa siku ni mechi ya ligi pamoja na mechi za Champions League. Tunaamini bado tuna siku tano au sita za kuendeleza tulichokianza,.Hii itakuwa mechi ngumu na tunahitaji matokeo kadiri inavyowezekana.” amesema
VISA, TAIFA VYAWAKWAMISHA
Katika hatua nyingine, Rweyemamu amefichua kuwa Simba ilikumbana na changamoto kadhaa kambini, ikiwemo masuala ya visa vya kuingia Afrika Kusini pamoja na kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa.
“Ukiunganisha na wale waliokuwa kwenye National Team, kiukweli kuingia kulikuwa na mfumo ambao ulitupa changamoto, lakini tulikuwa na wachezaji,” amesema.
Ameeleza kuwa licha ya changamoto hizo, Simba iliweza kuendelea na programu yake kutokana na kuwa na idadi ya kutosha ya wachezaji.
“Mwisho wa siku kanuni inataka wachezaji 40, hivyo unaweza kukuta mchezaji yupo siku ya mechi fulani na siku nyingine hayupo. Lakini sisi tunaamini tulichokuja kukipata tumekipata kwa asilimia kubwa,” amesema.
SI MATOKEO, NI ‘COORDINATION’
Rweyemamu pia amefafanua kuwa baadhi ya michezo iliyochezwa Afrika Kusini haikuwa mechi za kawaida za kirafiki, bali ilikuwa mechi za kirafiki za mazoezi zilizolenga zaidi kuwapa makocha nafasi ya kutathmini utekelezaji wa maelekezo ya kiufundi na uelewano wa wachezaji.
“Michezo ya kirafiki ilikuwa ya kiufundi, ndiyo maana inachezwa asubuhi na zikiwa ndani. Taratibu zake zinatofautiana. Unaweza kukuta tumecheza dakika 30 kila kipande au dakika 20 kwa 20, na tulikuwa tunachanganya namba ili kila mtu apate namba ya kucheza,” amesema.
Ameongeza “Sisi hatukuwa tunatafuta matokeo. Tulikuwa tunaangalia kile ambacho tumejifunza kimeingia kwa wachezaji, kama uratibu baina ya wachezaji.”
SIMBA YAREJEA, OCTOBER YAWASUBIRI
Simba sasa inarejea Tanzania ikiwa na siku chache za mwisho za maandalizi kabla ya kuingia kwenye ratiba nzito ya Oktoba, ikiwemo Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga na majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rweyemamu anaamini kazi iliyofanyika Afrika Kusini imewapa kile walichokihitaji kwa asilimia kubwa, lakini sasa jukumu linahamia uwanjani ambako Simba inapaswa kutafsiri maandalizi hayo kuwa matokeo.