Friday, January 16, 2026
Home Blog

SIMBA INAFANYA VITENDO SIO MANENO, MANGUNGU

0

MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amesema maandalizi ya timu hiyo yanaendelea vizuri huku hatua zote muhimu zikifanyika kwa kuzingatia mpango na utaratibu walioujiweka, sambamba na mahitaji ya benchi jipya la ufundi linaloongezwa nguvu chini ya kocha Steve Berker.

Mangungu amesema hadi sasa hakuna jambo linalowapa wasiwasi viongozi wa klabu hiyo, kuwa hali hiyo inaweza kuwa tofauti kwa baadhi ya mashabiki ambao wamekuwa na wasiwasi kutokana na kutokutangazwa rasmi kwa baadhi ya mabadiliko ndani ya timu.

Ameeleza kuwa klabu imeamua kufanyakazi kwa umakini na utulivu, badala ya kutoa taarifa za haraka, ili kuhakikisha kila hatua inayochukuliwa inaleta tija kwa maendeleo ya timu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa mujibu wa Mangungu, benchi la ufundi tayari limetoa maelekezo katika maeneo mbalimbali yanayohitaji maboresho, yote yakilenga kuongeza uwezo na ushindani wa kikosi cha Simba katika mashindano yanayoikabili.

Amesema uongozi unaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kwa umakini mkubwa, na kusisitiza kuwa tathmini ya kina itatolewa mara tu watakapokuwa tayari na mambo yatakapokamilika kikamilifu.

“Yapi maneno mengi yanayosemwa nje ya uwanja ambayo ni propaganda, lakini Simba haitapoteza muda kujibu maneno hayo, bali itaendelea kuthibitisha ubora wake kwa vitendo, si maneno,” Amesema.

SINGIDA BLACK STARS KUTUMIA MBILI BARA KUJIWEKA

0

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema mechi mbili za Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji na JKT Tanzania watazitumia kama njia ya kujiweka tayari kwa ajili pambano la michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Otoho ya Jamhuri ya Congo Brazzaville.

Mechi hiyo ya CAF inatarajiwa kupigwa Januari 25 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ambapo Singida itakuwa ikisaka ushindi wa kwanza ikiwa Kundi C katika mechi mbili za awali za kundi hilo ilipoteza mbele ya CR Belouizdad ya Algeria kisha kutoka sare ya 1-1 na Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwa sasa imeweka kambi jijini Dar es Salaam ikijiandaa na mechi za Ligi Kuu inayorejea baada ya kusimama kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea kule Morocco.

Kwa mujibu wa ratiba mpya, Singida inatarajiwa kucheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kesho Ijumaa dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kurudia tena uwanjani Januari 20 dhidi ya maafande wa JKT Tanzania inayoongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 17.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Ouma amesema baada ya kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2026, timu imeendelea kujifua kwa ajili ya michuano iliyo mbele yao na lengo likiwa ni kuona wanakuwa bora zaidi.

“Timu inaendelea vizuri na kwa mujibu wa ratiba tutakuwa na mechi mbili za ligi kabla ya michuano ya kimataifa, hivyo tutazitumia hizo kuhakikisha tunakuwa bora kabla ya kuivaa AS Otoho d’Oyo,”  amesema Ouma na kuongeza;

“Ninachofurahia ni kwamba timu ipo kwenye hali nzuri ya utimamu baada ya kutoka kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kukosa baadhi ya wachezaji sasa timu imekamilika na inaendelea na maandalizi.”

Kocha huyo raia wa Kenya, aliyechukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyepandishwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo huku akiendelea kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars, amesema anatarajia kupata ushindani wa kutosha kutoka kwa Dodoma Jiji na JKT Tanzania timu hizo ndio zitakazotoa picha ya timu yake itaikabiri vipi AS Otoho ikiwa uwanja wa nyumbani.“Ligi yetu ni bora na yenye ushindani, ilianza vyema msimu huu nafikiri kutakuwa na muendelezo bora baada ya kurejea tena, sitarajii mechi rahisi hata wachezaji wanatambua hilo hivyo tunafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunakuwa bora na imara tayari kwa ushindani.”

Singida iliyotolewa nusu fainali ya Mapinduzi 2026 na Yanga iliyobeba ubingwa juzi usiku kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, kwa sasa inashika nafasi ya 12 katika Ligi Kuu ikiwa na pointi nane kupitia mechi tano.

Katika michuano ya Shirikisho Afrika inashika mkia katika Kundi C ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili ikiambulia sare moja na kupoteza mbele ya CR Belouizdad yenye alama tatu ikiwa ya tatu nyuma ya As Otoho na Stellenbosch zenye pointi nne kila moja kwa sasa.

Singida itacheza na As Otoho mechi mbili mfululizo, kwani baada ya kuwa wenyeji Januari 25 itasafiri kuifuata jijini Brazzaville kuruidiana kabla ya kujiandaa kumalizia mechi mbili za mwisho za kundi dhidi ya Stellenbosch na Belouizdad ili kusaka tiketi ya robo fainali.

FERUZ WA SIMBA AREJEA LIGI KUU

0

KIPA wa zamani wa Simba, Ahmed Feruz amerejea katika Ligi Kuu Bara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuidakia Namungo akitokea Stand United inayoshiriki Ligi ya Championship.

Kabla ya kuitumikia Stand United, Feruz alikipiga Kagera Sugar kwa mkopo wa miezi sita akitoka Simba ambako hakuwa anapata nafasi ya kucheza.

Mmoja wa viongozi wa Namungo (hakutaka kutajwa jina) aliliambia Mwanaspoti, klabu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda, imemsajili Feruz ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi, hususan eneo la ulinzi.

Mmoja wa watu wa karibu wa Feruz (jina tunalo) amesema kipa huyo ameamua kujiunga na timu hiyo ili aweze kucheza ligi kuu na kuonyesha uwezo wake.

“Namungo ni timu yenye mipango mizuri na ameridhishwa na mazungumzo waliyofanya, anaamini kama atapata nafasi basi anaweza kurudi kwenye kiwango chake.”

Inaelezwa usajili wa kipa huyo ni pendekezo la kocha mkuu, Juma Mgunda ambaye anamfahamu tangu alipokuwa anaifundisha Simba.

Namungo kwa sasa ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 12 kuopitia mechi nane ilizocheza, ikishinda tatu, kutoka sare tatu na kupoteza mbili ikiwa na makipa Jonathan Nahimana, Mussa Malika na Suleiman Said.

WAGOSI WAPO TAYARI KWA VITA LIGI KUU

0

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya amesema wachezaji wa timu hiyo wapo tayari kuendeleza vita na ushindani mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kurejea tena huku akitamba keshokutwa Jumamosi watakitonesha kidonda cha Azam FC ilitoka kufungwa katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 mbele ya Yanga waliobeba taji kwa penalti 5-4.

Wagosi wa Kaya waliopo nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu ikicheza mechi nane na kuvuna pointi tisa, watakuwa ugenini kukabiliana na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex, pambano likipangwa kupigwa kuanzia saa 1:00 usiku.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Muya akisema hawatarajii mechi rahisi kutokana na ushindani uliopo lakini wamejiandaa kupambania pointi tatu ugenini ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.

“Hakuna kinachoshindikana mpira ni mchezo wa makosa dakika 90 zenye mbinu bora na sahihi zitatupa matokeo mazuri ugenini tunaheshimu ubora wa wapinzani wetu na wao wasitarajie mteremko kutoka kwetu,” amesema Muya na kuongeza;

“Tunafahamu imetoka kupoteza taji la Mapinduzi kwa mikwaju ya penati hawatataka kurudia makosa kwa kupoteza pointi tatu Ligi kuu na sisi tumejiandaa kuonyesha ushindani dhidi yao hivyo utakuwa mchezo mzuri na wa ushindani.”

Kocha huyo alisisitiza; “Tutaingia kwa tahadhari na kuwaheshimu wapinzani wetu ni timu ambayo ina historia ngumu kwetu tangu imepanda tukikutana huwa mchezo unakuwa mgumu timu bora ndio inaamua matokeo.”

“Tunatarajia mechi ngumu na ya ushindani tumejiandaa vizuri na tunatarajia matokeo mazuri kwenye mchezo wa huo kutokana na mipango ya benchi la ufundi sambamba na wachezaji wenyewe,” aliongeza.

Rekodi inaonyesha katika mechi ya mwisho uwanjani hapo msimu uliopita timu hizo zilipokutana katika Ligi Kuu, wenyeji Azam ilishinda kwa bao 1-0 na ziliporudiana zilitoka suluhu, lakini katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii 2024, Azam iliifunga Coastal 5-2

PHIRI AKWAMBA ULAYA AIBUKIA ZIMBABWE

0

MSHAMBULIAJI nyota wa Singida Black Stars, Mzambia Andrew Phiri amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Hard Rock FC inayoshiriki Ligi Kuu Zimbabwe, baada ya dili lake kwenda Ureno kufanya majaribio kukwama.

Nyota huyo alikwenda Ureno katika timu ya Clube Desportivo Nacional, baada ya uongozi wa kikosi hicho kuridhia kwa lengo la kwenda kujaribu bahati yake Ulaya, ingawa baada ya kutofanikiwa amepelekwa Hard Rock ya Zimbabwe kwa mkopo.

Phiri aliyejiunga na Singida, Agosti 26, mwaka jana akitokea Maestro United ya Zambia na mkataba alionao na timu hiyo utafikia tamati rasmi Juni 30, 2028, ingawa baada ya ushindani wa nafasi katika kikosi hicho mabosi wameona ni vyema wamtafutie timu nyingine.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti Phiri bado ni mchezaji mzuri anayeweza kukisaidia kikosi hicho, ingawa baada ya majadiliano kati yao na kambi ya nyota huyo wameona ni vyema wamtafutie klabu itakayompa zaidi nafasi.

Phiri aliyezaliwa Mei 21, 2001, alifanya pia majaribio Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini Machi 2025, ambapo nyota huyo alimaliza mfungaji bora wa Maestro United kwa misimu minne mfululizo, huku akiifungia mabao 69, kwenye mashindano yote.

Mwanzoni mwa msimu, nyota huyo alikuwa anahusishwa na timu za Zesco United na Power Dynamos zote za kwao Zambia, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kilichoivutia miamba hiyo, huku kwa msimu wa 2023-2024, akichaguliwa mchezaji bora wa msimu.

Pia, mshambuliaji huyo kabla ya kujiunga na Singida msimu huu, alikua akihusishwa na miamba wa soka hapa nchini Yanga, Simba na Azam, kisha Pamba Jiji kuingilia kati dili hilo na kushindwa kumudu fedha zilizohitajiwa na Maestro United na kuibukia kwa Wauza Alizeti hao.

MPANZU ATANGAZA HATARI JUMAPILI

0

NYOTA wa Simba SC, Elie Mpanzu, ameonyesha kiwango kikubwa cha hamasa na ari ya kupambana kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumapili.

Kiungo huyo ameweka wazi kuwa yuko tayari kutoa kila alichonacho kwa ajili ya timu na mashabiki wake, akiahidi kiwango cha juu uwanjani.

Simba inatarajia kuikabili Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kabla ya safari ya kwenda Tunisia kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa Januari 24.

Mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar wanaocheza Jumapili unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kujenga morali ya kikosi.

Kupitia ujumbe aliouchapisha, Mpanzu amesema ana motisha ya hali ya juu na hawezi kusubiri siku ya Jumapili kufika ili kuingia uwanjani na kutekeleza kile alichokijiandaa kwa muda mrefu.

Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa kurejesha tabasamu na furaha kwa Wanasimba waliokuwa na matarajio makubwa kwa timu yao.

Mpanzu ameongeza kuwa anatambua vyema shinikizo na matarajio ya mashabiki wa Simba, jambo linalompa nguvu ya ziada ya kujituma zaidi kila siku mazoezini. Kwa mujibu wake, dhamira ya kikosi ni kuhakikisha kinapata matokeo chanya na kuonyesha ushindani wa kweli.

Kiungo huyo amesisitiza kuwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ni muhimu si kwake binafsi tu, bali kwa timu nzima, kwani ni fursa ya kuonyesha umoja, mshikamano na kiu ya ushindi waliyonayo kama familia moja ya Simba SC.

Mpanzu amewahakikishia mashabiki kuwa yeye pamoja na wenzake wako tayari kupambana kwa nguvu zote uwanjani, wakilenga kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi na kupigania heshima ya klabu.

Amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu, akisisitiza kauli mbiu ya “Mabingwa Wekundu” kama ishara ya imani na matumaini ya ushindi mkubwa Jumapili.

MBWA MWITU AINGIA RASMI NDANI YA YANGA

0

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Radomiak Radom ya Poland, Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu kwa jina la Mbwa Mwitu (Depu), ametambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa klabu ya Yanga SC, hatua inayoongeza nguvu mpya katika kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Depu amesajiliwa katika dirisha dogo la usajili kwa lengo la kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Yanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa klabu hiyo kuongeza ushindani na ufanisi kuelekea nusu ya pili ya msimu. Ujio wake unaashiria dhamira ya dhati ya Yanga kuendelea kuwa imara ndani na nje ya nchi.

Mshambuliaji huyo raia wa Angola anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Yanga katika dirisha hili dogo, akijiunga na Emmanuel Mwanengo, Mohammed Damaro pamoja na Allan Okello ambaye alitambulishwa rasmi siku chache zilizopita.

Ujio wa Depu pia unaambatana na kurejea kufanya kazi chini ya kocha wake wa zamani, Pedro Goncalves. Hali hiyo inaaminika itamsaidia mchezaji huyo kuzoea kwa haraka falsafa ya timu, mfumo wa uchezaji pamoja na mahitaji ya benchi la ufundi.

Yanga imeendelea kuonesha nia thabiti ya kuboresha kikosi chake ili kudumisha ushindani katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa. Usajili wa Depu unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji na kutoa chaguo zaidi kwa benchi la ufundi.

Kwa uwezo wake mzuri wa kufumania nyavu akiwa anacheza nafasi ya namba tisa, Laurindo ‘Depu’ anatarajiwa kuwa silaha muhimu kwa Yanga, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona mchango wake ndani ya uwanja.

FUNZO LA UKIMYA ANAREJEA KAZINI, SINGANO

0

BAADA ya kimya kingi cha aliyekuwa winga wa Simba, Azam FC na TP Mazembe, Ramadhan Singano anasimulia kilichomuweka nje ya uwanja na utayari wake wa kurejea kazini kwa sasa.

Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Singano maarufu hapa nchini kwa jina la Messi anasema kuna funzo alilopata katika ukimya wake, hasa jinsi ya kuishi na jamii.

“Ukiwa unacheza, unatumia muda mfupi sana kushirikiana na jamii, lakini kwa muda niliokaa na jamii nimejua ina picha gani kunihusu,” anasema mchezaji huyo.

Anasema mastaa wanaotamba kwa sasa ni vizuri wakajua kuna maisha mengine yatakayotafsiri matendo yao ya sasa, hivyo anawashauri waache picha sahihi katika jamii.Anasimulia kilichokuwa nyuma ya ukimya wake kuwa ni masuala ya kimkataba baina yake na TP Mazembe aliyojiunga nayo msimu wa 2019/20 akitokea Azam FC.“Nilijiunga na TP Mazembe kwa mkataba wa miaka mitano. Ilikuwa 2019/20. Yapokuna mambo hayakwenda sawa baada ya wao kunitoa kwa mkopo kwenda Nkana ya Zambia mwaka 2021, hadi Fifa ikaingilia kati. Tayari tulishamalizana mwaka jana; nipo tayari kuendelea na maisha yangu mengine, kwa sasa nipo huru,” anasema.Je, anajuta kujiunga na TP Mazembe? Nyota huyo anafafanua hilo kwa maana mbili; ameondoka na funzo la namna klabu hiyo ilivyokuwa imewekeza na ushindani ulivyokuwa mkubwa, kwani mchezaji anayepata nafasi ya kucheza ni yule aliye na kiwango cha juu.“Tulijiunga TP Mazembe kipindi hicho walikuwepo wachezaji wenye majina makubwa Afrika, kama kipa Robert Kidiaba, hadi aliwahi kupewa Uwaziri wa Michezo wa DR Congo. Mtu kama huyo ujue alifanya makubwa hadi serikali ya nchi hiyo ikaona ana kitu cha kuchangia katika sekta hiyo.”

Anaongeza kuwa, “nilibahatika kukaa naye karibu, na alikuwa anatuona kama ndugu zake. Kwa kile ambacho Mbwana Samatta alikifanya, kiliacha alama ya Watanzania kuaminika. Kikubwa zaidi, nilijifunza uvumilivu na nidhamu kutoka kwake.

“Ushindani uliokuwepo ulinitafsiri thamani ya kiwango na upambanaji wangu nje ya nchi; hivyo katika hilo nilifaidika. Labda upande wa changamoto ni ukimya, kwani watu walikuwa hawajui nipo wapi na kwa nini, baada ya kutokea tofauti ya kimkataba baina yangu na wao.”

Anasema kitendo cha TP Mazembe kumtoa Nkana kwa mkopo kilitokana na shauku yake ya kupata timu ya kucheza, lakini changamoto ikawa ni ukiukwaji wa baadhi ya vipengele vilivyokuwapo katika mkataba, vikafanya ndoto yake iishie njiani na ikawa chanzo cha kurejea Tanzania.

“Isingekuwa changamoto hiyo, ningekuwa bado nipo uwanjani kama ambavyo wenzangu wanacheza, kama Seseme (Abdallah), Ndemla (Said), Mkude (Jonas) na wengine wengi. Ikitokea nafasi, nitarejea kukamilisha deni nililonalo la kuendelea kukitendea haki kipaji changu,” anasema.Anathibitisha zipo faida na hasara kwa mchezaji anayetaka kuendelea na ndoto za mpira wa miguu kufanya mazoezi nje ya timu kwa muda mrefu, kwani atakuwa anakosa kujiamini wakati wa mechi za mashindano.

“Sikuwahi kuacha kufanya programu ya mazoezi. Wakati mwingine nacheza mechi za mtaani ili kulinda kiwango changu, lakini huwezi kufananisha na wanaocheza Ligi Kuu, ambao muda wote wanajifunza mbinu za makocha na ushindani wa namba baina yao na timu pinzani,” anasema Singano, na kuongeza:

“Faida ni kwamba nimejifunza vitu vingi vya maisha nje ya kazi hiyo. Nimepata muda wa kusimamia miradi yangu ninayowekeza, na kuibua ndoto za wachezaji wengine kupitia kituo changu. Tayari kuna kipa anaitwa Daniel; kuna kituo kingine ambacho nimempeleka Mwanza.”

Singano anatamani siku zingerudi nyuma apate nafasi nyingine ya kufurahia maisha ya Simba B, walivyoishi kwa umoja, upendo na nguvu ya kuzipambania ndoto zao.

“Kiuchumi nitasimulia Simba ya wakubwa, maana zipo baadhi ya hatua nilizozipiga, ila maisha nisiyoyasahau ni ya Simba B. Tulijengwa katika upambanaji na upendo; hadi sasa tunawasiliana na kutafutana. Natamani itokee nafasi nyingine yajirudie,” anasema Singano, na kuongeza:

“Tulikuwa tunatamani ile Simba B ihamishwe, wachezaji wote waende timu moja halafu tukakabiliane na wapinzani. Ukiachana na sisi ambao tulijulikana kama Hassan Isihaka, Said Ndemla, Abdallah Seseme, Jonas Mkude na Edward Christopher, wapo wengine wengi waliokuwa na vipaji vikubwa mno.”

Mbali na hilo, amekiri kujifunza kitu kikubwa katika uhamisho wake wa kutoka Simba aliyojiunga nayo mwaka 2011 na kutua Azam mwaka 2015: “Nilijifunza utulivu na ukimya, kwa sababu maneno yalikuwa mengi; mashabiki baadhi hawakunielewa, lakini maisha ya mchezaji ndivyo yalivyo.”

Anaongeza: “Ndiyo maana hata nilipopata changamoto na TP Mazembe, hakuwahi kusikia nikizungumza popote; nilikaa kimya. Ukicheza timu iliyo na mashabiki halafu ukapendwa, ikitokea unahama wanakuona kama msaliti. Sasa hapo ilikuwa Simba kwenda Azam; vipi ingekuwa Simba kwenda Yanga, au mchezaji aliyeko Yanga kwenda Simba? Lazima atapata changamoto ya kuchukiwa. Jambo la msingi ni wajifunze kukaa kimya.”

Anasema maisha ya Azam yalikuwa mazuri na yalimfungulia milango ya kwenda kujifunza soka la kimataifa: “Nilitokea Azam kwenda TP Mazembe, kisha Nkana. Pia zipo hatua za kiuchumi nilizozipiga kwa kile ambacho nilikipata, ingawa sitaweza kutaja kitu kimoja baada ya kingine.”

Anasema ingawa akiangalia Ligi Kuu anaviona vipaji vikubwa na ushindani, inakuwa ngumu kwake kueleza anatamani kucheza na nani hadi apate nafasi ya kuingia uwanjani na kuuona uhalisia, tofauti na aliowahi kufurahi kucheza nao kipindi cha nyuma.

“Nilikuwa nikicheza na kaka zangu kama Haruna Moshi ‘Boban’, Amri Kiemba, na wenzangu wengine Seseme na Salum Abubakar ‘Sure Boy’. Nilikuwa nanaf urahia, kwani ni mafundi, ila wapo wengi; kwa kifupi hao ni baadhi,” anasisitiza, akisema aliyekuwa anamkubali tangu akiwa mtoto ni Boban.Anasema vitu ambavyo hatakaa avisahau ni kupandishwa kutoka timu B kwenda Simba A. Uchungu alioupata ni kukosa mishahara ya miezi mitatu: “Baada ya kupanda, nikatamani niachane na soka. Kaka zangu walisema napaswa kuongeza bidii nitaanza kufurahia kipaji changu, na maneno yao yalitimia baada ya kuyazingatia. Jambo lingine nilipata nafasi ya kuitumikia Taifa Stars.”

Anasema nje ya mpira wa miguu anapendelea kusoma vitabu vyenye mafunzo, akikitaja kimojawapo kuwa ni Watoto wa Mama Ntilie, kilichojaa mafunzo ya kweli ya mtaani.

“Watu tulikotokea maisha ya chini, hicho kitabu ukikisoma kina funzo, tofauti na watoto wa ushuani. Napenda kusoma vitabu mbalimbali ili kupanua uwezo wa kufikiri na kutafsiri vitu katika jamii,” anasema.

Singano anakumbuka akiwa mdogo alikuwa akienda na wenzake majalalani kuokota mkaa; kisha akiukusanya mwingi anapeleka nyumbani. Wakati mwingine anauza ili kupata fedha ya kujikimu au kumpa mama yake mzazi kusaidia nyumbani.

“Tunaenda ambako gari la mkaa limeshuka, tunaokota uliobaki; wakati mwingine mpaka majalalani. Kifupi, nimepitia mengi, lakini nashukuru Mungu hapa nilipo sasa haikuwa rahisi hadi Watanzania kunifahamu. Jambo ninalolitamani ni wazazi wangu wangekuwa hai, wangekula kidogo nilichokipata,” anasema Singano, akiwa mtoto wa mwisho kati ya sita; kaka zake wakiwa ni Khamis, Moghammed na Bakari, huku wawili wakitangulia mbele ya haki.

SIMBA WAINGIA SOKONI KUSAKA KIMYA MPYA

0

UONGOZI wa klabu ya Simba umeingia sokoni kutafuta kipa mwingine wa kuziba pengo lililosababishwa na majeraha ya makipa wao Moussa Camara na Yakubu Seleman, hali ambayo imeifanya timu hiyo kubaki na chaguo finyu langoni.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema uwezekano wa Camara kuchelewa kupona pamoja na Yakubu kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja au miwili, umeilazimu klabu kuanza mchakato wa kusaka kipa mbadala.

Ahmed amesema Simba haiwezi kujiweka katika hatari ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mzunguko wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na kipa mmoja pekee, Abel Hussein, anayesaidiwa na makipa wawili kutoka timu ya vijana.

Amefafanua kuwa timu inahitaji kipa mwenye uzoefu mkubwa ili kuhakikisha usalama wa lango na kuongeza ushindani ndani ya kikosi.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kwa mujibu wa ripoti za awali za kitabibu, Camara anaendelea vizuri na anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa mwezi huu wa Januari.

“Hadi sasa sijapokea taarifa yoyote mpya inayobainisha kama Camara atarejea mwezi huu au kama kutakuwa na mabadiliko yoyote katika matibabu yake,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa kurejea kwa Camara kutachelewa zaidi, basi Simba haina budi kumsajili kipa mwingine ili kuhakikisha timu inakuwa na uhakika na uimara wa kikosi chake kwa mashindano yanayoikabili.

Kuhusu hali ya Yakubu Seleman, Ahmed amesema bado hajapata ripoti kamili kutoka kwa jopo la madaktari, akisisitiza kuwa baada ya kurejea kutoka AFCON watatoa taarifa rasmi kwa mashabiki wa Simba ili kuwaondoa hofu na wasiwasi.

OKELLO ANA MZUKA YANGA, AANZA KAZI GYM

0

HAKUNA kulala, hilo ndilo neno linaloelezea mwanzo wa safari ya mshambuliaji mpya wa Yanga, Allan Okello, ambaye tayari ameanza rasmi mazoezi na kujiunga na wachezaji wenzake katika Gym mara baada ya kukamilisha usajili wake.

Okello ameonekana akiwa na hamasa kubwa na ari ya hali ya juu wakati wa mazoezi, akionesha wazi kuwa yupo tayari kukabiliana na changamoto mpya ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuipigania nafasi yake ndani ya kikosi cha Wananchi.

Mshambuliaji huyo amesajiliwa akitokea klabu ya Vipers SC ya Uganda, akiwa na uzoefu mpana wa soka la Afrika Mashariki pamoja na mashindano ya kimataifa, jambo linaloongeza matumaini kwa benchi la ufundi la Yanga.

Ujio wake unatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Wananchi, huku kocha akiamini kuwa kasi, ufundi na uwezo wake wa kufumania nyavu vitakuwa silaha muhimu kwa timu msimu huu.

Okello pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes, na anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliowahi kung’ara katika Ligi Kuu ya Uganda pamoja na michuano ya klabu barani Afrika.

Mashabiki wa Yanga tayari wameanza kuweka matumaini makubwa kwake, wakitarajia kumuona akitoa mchango mkubwa katika jitihada za kutetea ubingwa wa ligi na kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu.

329,001FansLike
12,344FollowersFollow
16,900SubscribersSubscribe

EDITOR PICKS