
WAKATI dirisha dogo la usajili likiwa limefunguliwa, Kocha mpya wa Simba, Steve Barker, ameweka msimamo wake wazi kwa kuutaka uongozi wa klabu hiyo kutokurupuka kufanya usajili wala kuuza wachezaji hadi atakapokamilisha tathmini yake ya kikosi.
Barker amesema anahitaji muda wa kutosha kuwatazama wachezaji waliopo kikosini ili kupata picha halisi ya ubora, udhaifu na mahitaji ya timu, kabla ya kufanya maamuzi yoyote muhimu yanayohusu mabadiliko ya kikosi.
Kocha huyo anazitumia vyema mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea Visiwani Zanzibar kama jukwaa la kufanya tathmini ya kina kwa wachezaji wake, akilenga kubaini aina ya wachezaji anaohitaji kwa falsafa na mfumo wake wa uchezaji.
Kupitia mashindano hayo, Barker anatazamia kuona uwezo wa wachezaji katika mazingira ya ushindani, jambo litakalomsaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu nafasi zinazohitaji kuimarishwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Hata hivyo, taarifa zinaeleza kuwa kuna baadhi ya wachezaji waliopo kwenye orodha ya wanaoweza kuuzwa, akiwemo Jean Charles Ahoua, ambaye inadaiwa anawindwa na klabu ya Raja AC ya Morocco.
Raja AC inanolewa na aliyekuwa Kocha wa Simba, Fadlu Davids, hali inayoongeza uzito wa tetesi hizo, ingawa bado hakuna uamuzi rasmi uliotolewa kuhusu mustakabali wa kiungo huyo.
Chanzo cha ndani kimeeleza kuwa uongozi wa Simba umeamua kumuachia Barker jukumu zima la kuishauri klabu kuhusu usajili, ili kuhakikisha maamuzi yatakayofanyika yanazingatia mahitaji halisi ya timu na malengo ya muda mrefu ya klabu hiyo.