Home Uncategorized TPL NDO ISHAISHA HIVYO, HIYO RATIBA YA FA INATISHA

TPL NDO ISHAISHA HIVYO, HIYO RATIBA YA FA INATISHA


BINGWA ndo kama alivyoshinda na Ligi Kuu Bara imemalizika huku timu nyingi zikiwa zimeambulia maumivu makubwa msimu huu.

Ilikuwa ni aina moja ya ligi iliyokuwa na ushindani kwa timu chache ambazo zilikuwa zinashiriki ligi hali iliyopoteza ule mvuto na msisimko ambao ulianza awali.

Kukosekana kwa mdhamini kumeziminya klabu nyingi na kufanya uendeshaji kuwa mikononi mwa viongozi wenyewe huku wachezaji wakitumia nguvu kubwa kupambana kwa ajili ya timu.

Bodi ya Ligi imekuwa ikifanya mambo mengi ambayo yanajirudia jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya soka letu hasa kwa upande wa mpangilio mzima wa ratiba pamoja na waamuzi.

Ni somo kubwa ambalo timu imezipata msimu huu pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuna jambo ambalo nina amini watakuwa wamejifunza licha ya kuwa wamekamilisha msimu kama ambavyo walikuwa wanataka iwe.

Kama hatutaambiana ukweli tutazidi kuumizana hasa linapokuja suala zima la kuwa na ligi bora tena yenye ushindani ni lazima tuwekeze kwa waamuzi bora pamoja na ratiba rafiki.

Itakuwa ni jambo la kushangaza mambo ambayo yametokea msimu huu yakatokea tena msimu ujao hilo nawaachia TFF wenyewe wafanye kazi kwa ukaribu kutatua changamoto za ligi.

Mashabiki wanapenda kuona ligi yenye ushindani inayovutia kuitazama kila siku na sio kila baada ya mechi kuisha mtu unajutia kwa nini ulipoteza muda wako.

Maboresho yaanze kuanzia ndani ya uwanja na kabla ya mechi, kila mechi ipewe kipaumbele sawa bila kubagua aina ya timu kama tabia hii itaendelea ule ufalme wa Uyanga na Usimba itakwa ngumu kupotea.

Nirudi kwenye jamvi la leo ambapo ningependa kuzungumza kuhusu fainali ya FA ambayo itachezwa Juni Mosi uwanja wa Ilulu mkoani Lindi bado kuna mengi ya kutazama hapa.

Jambo la kwanza ni muda wa fainali kuchezwa ni mfupi sana baada ya ligi kuisha maana kama ligi inaisha Mei 28 hakukuwa na haja ya kutumia siku tatu kwa ajili ya maandalizi.

Ukitazama Lipuli ambayo inatoka Mbeya itatumia siku mbili kwa ajili ya safari njiani maana mchezo wake wa mwisho utakuwa hapo imecheza na Tanzania Prisons, uwanja wa Sokoine.

Kwa maana hiyo safari imeanza tarehe 29 mpaka 30 kuibukia Lindi kwa ajili ya kucheza hiyo fainali huku wakiwa na muda wa kujiaandaa wa siku moja pekee hii haijakaa sawa.

Timu haitakuwa na muda wa kufanya maandalizi zaidi ya kupumzika kwa ajili ya kusubiri mchezo na kufanya mazoezi ya mwisho siku moja hii haijakaa vizuri.

Kwa mlolongo huo itakuwa ngumu kwa wachezaji kuonyesha ule uwezo ambao wapo nao pamoja na kandanda la ushindani ambalo limezoeleka kutolewa na timu.

TFF ilipaswa kuipa timu muda wa kujipanga ili kuwapa nafasi mashabiki kujiandaa kuipa sapoti timu kwa kuwa ni muda mfupi kwa mashabiki kutoka sehemu kwenda sehemu nyingine.

Mwaka jana ilikuwa tofauti kwa Mtibwa na Singida walicheza mchezo wao katika mazingira safi iliyofanya kumpata mshindi wa haki kwa wakati sahihi.

Pia hata suala la uwanja inaonekana ni mikakati ya kisiasa ambayo inaingizwa kwenye soka jambo ambalo sio sawa linamaliza ubora wetu wenyewe na hadhi ya mashindano.

Tujifunze kwa wenzetu Uingereza lazima fainali ya FA ichezwe Wembley, maana yake nini mchezaji anakuwa anaona fahari kucheza kwenye uwanja mkubwa wenye hadhi sawa na mashindano yenyewe. 

Sasa leo tunasema fainali Lindi, uwanja wa Ilulu bado haujawa na hadhi ya kimataifa, unapozungumzia fainali ya FA sio kitu kidogo kama ambavyo wengine wanafikiria.

Kwa hilo  bado inaishusha hadhi ya fainali hasa ukizingatia kwamba mshindi anapata nafasi ya kuwakilisha Taifa kwenye mashindano ya Kimataifa hili linaumiza.

Kuna vitu vya kutazama, wanadai wanakwenda kufanya ukaguzi wa uwanja, hii inafurahisha maana kama mnatambua kuna fainali kisha mnatangaza uwanja bila kufanya ukaguzi hili ni jambo la ajabu.

Pia ukitazama ubora wa uwanja wenyewe hautoi fursa kwa mashabiki kuona soka likipigwa kwa usawa hasa kwa kukosekana kwa majukwaa kwenye uwanja hili lichukuliwe hatua.

Ifike wakati iwe inajulikana kwamba kama ni fainali ya FA lazima ifanyike kwenye uwanja wa Taifa kwa kuwa una hadhi ya kimataifa itatoa heshima kwa timu ambazo zinashiriki michuano hiyo.

Muda ni sasa wa TFF kufanyia maboresho haya matatizo ambayo yanajitokeza mara kwa mara na kusimamia vitu vya soka kwa utaratibu ambao unaleta matokeo bora.

Kila kitu kinawezekana endapo tutaamua mwisho wa siku suala la ratiba nalo linapaswa litazamwe kabla ya kupanga mechi ambazo ni muhimu kwa kila timu kupata ushindi.

SOMA NA HII  KIKOSI CHA SIMBA KITAKACHOANZA LEO DHIDI YA GWAMBINA FC