Home Uncategorized KAMATI MPYA YA USAJILI YANGA NOMA

KAMATI MPYA YA USAJILI YANGA NOMA


KAMATI ya usajili wa Yanga bado ni siri kubwa na huenda ikatangazwa wikiendi hii lakini Spoti Xtra limenasa majina ya vigogo waliopo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, kamati hiyo inaundwa na mabosi wengi wanaojiweza kifedha na mipango ya ndani na nje ya uwanja chini ya Mwenyekiti wake, Franck Kamugisha.

Spoti Xtra limebaini kwamba, anasaidiwa na Ahmad Islam ambaye mfanyabishara mkubwa mkoani Morogoro, Samwel Rupia, Rogers Gumbo, Samwel Lucqumay, Moses Katabaro.

Wengine ni Abdallah Bin Kleb na Lucas Mashauri. Mmoja wa viongozi wa Yanga alidokeza kwamba kamati hiyo wamepanga iwe siri hadi usajili utakapomalizika ili ifanye kazi yake kwa uhuru na kuepuka kusumbuliwa na wanachama na mashabiki pamoja na madalali wa wachezaji.

“Lengo ni kuona usajili unafanywa kwa siri bila ya kuingiliwa huku wakikwepa fitna za watani wetu Simba. “Kama unavofahamu timu haina fedha, hivyo ni lazima usajili ufanywe kwa siri kwa kuificha kamati husika,” aliongeza mmoja wa viongozi wa Yanga na kusema safari hii watatengeneza kikosi makini.

Viongozi wa juu wa Yanga jana hawakuwa tayari kutoa ufafanuzi kuhusiana na ishu ya kamati lakini walikiri ipo na inachapa kazi. Yanga wamepania kuifumua timu hiyo na kuisuka upya chini ya Kocha Mwinyi Zahera ambaye atashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Agosti.

CAF WIKI MBILI

Caf imewapa wawakilishi wote wa Tanzania akiwemo Yanga hadi Juni 30 kukamilisha na kuwasilisha usajili wote wa wachezaji kwa ajili ya michuano ya kimataifa inayoanza Agosti.

Hiyo inamaanisha kwamba ndani ya wiki ijayo Yanga ambao wamepata nafasi ya dezo ya kushiriki michuano ya msimu ujao watapaswa kuwa wamekamilisha usajili wao. Simba na Yanga zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam na KMC zikishiriki Shirikisho. Tanzania imeongezewa timu kutokana na ufanisi wa Simba kimataifa msimu uliopita.

CHANZO: SPOTI XTRA

SOMA NA HII  JOHN BOCCO NDIO BASI TENA BENCHIKHA AMKATAA HADHARANI