MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu leo Juni ameendesha harambee maalum ya kuichangia timu ya taifa (Taifa Stars) katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inashiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Juni 21 hadi Julai 19 huko Misri.
Harambee hiyo ilizinduliwa rasmi Jumatatu iliyopita jijini Dar es Salaam na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na leo ndiyo kilele chake.
Katika hafla hiyo, Mama Samia amenunua jezi ya Taifa Stars kwa Sh. milioni 5.
Kampuni na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi zimechangia kupitia kununua jezi na wadau kadhaa wamejitokeza kununua jezi.
Mamlaka ya Kudhibiti Mawasiliano (TCRA) wamenunua jezi za sh. millioni moja, Benki ya CRDB imenunua jezi kwa sh. millioni moja, Kampuni ya mafuta ya ORYX nayo imenunua jezi kwa sh. millioni moja, na shirika la nyumba la taifa (NHC) limenunua za sh. milioni moja.
Kampuni ya Kamaka – wamenunua jezi kwa milioni mbili, na Benki ya KCB imenunua jezi kwa milioni 1.5.
Mbali na Samia, viongozi wengine waliohudhuria ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi.