Home Uncategorized JPM: MAKONDA UMESEMA UKIENDA MISRI TUTASHINDA? HAYA NENDA – VIDEO

JPM: MAKONDA UMESEMA UKIENDA MISRI TUTASHINDA? HAYA NENDA – VIDEO


RAIS John Magufuli amemruhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwenda nchini Misri kwa ajili ya kuipa hamasa timu ya taifa Tanzania (Taifa Stas) ili iibuke na ushindi dhidi ya Kenya baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa mabao 2-0 na Senegal juzi Jumamosi.

Magufuli ametoa ruhusa hiyo leo Jumanne, Juni 25, 2019, wakati akizindua Ghala na Mitambo ya Kuchakata Gesi ya LPG ya Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited katika eneo la Vijibweni Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Mwanzo wa Taifa Stars sio mbaya kwanza wamefungwa tugoli tuwili tu na timu kubwa kama ile nina imani watafanya vizuri. RC Makonda umesema ukienda Misri Taifa Stars tutashinda kutokana na motisha ya ushangiliaji, nakuruhusu panda ndege nenda.

“Na ukawaambie wachezaji wasikate tamaa, kwenye uwanja wa mpira kuna matokeo yote, unaweza kushinda au kushindwa, kawaambie wapambane, tunawaombea, ninaamini watashinda tu, sisi Watanzania tupo nyuma yao, kushinda kwao ni ushindi wa Tanzania nzima na kushindwa kwao ni kushindwa kwetu sote” amesema Rais Magufuli.

Awali RC Makonda alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi huo alisema; “Mimi ni mpenzi mkubwa wa Taifa Stars na nimeumizwa sana na matokeo ya Senegal, lakini kilichoniuma kikubwa zaidi ni watu kuwabeza wachezaji wa Taifa Stars ambao wameipa heshima nchi hii kwa miaka 39 kuingia AFCON 2019, leo wameonekana hawana afya njema, hawana chochote, hawana uongozi mzuri, hatuwezi kuwa na taifa la namna hii.

“Mheshimiwa Rais, kama itakupendeza ninaomba unipe ruhusa niende Misri kuwapa hamasa vijana wetu, nina uhakika watashinda mechi ijayo dhidi ya ndugu zetu Kenya. 

Vijana wetu wana ari kubwa ya ushindi, hata leo asubuhi nimeongea na nahodha Mbwana Samatta, amenihakikishia wapo vizuri na watashinda mechi ijayo,” amesema Makonda.

Mchezo wa taifa Stars na Kenya utapigwa keshokutwa Alhamisi, Juni 27, 2019.

SOMA NA HII  BARAKA MAJOGORO ATAJA SABABU YA KUTUMIA JEZI NAMBA 15