Home Uncategorized RASMI JINA LA KOTEI LATUA YANGA

RASMI JINA LA KOTEI LATUA YANGA


SIMBA na Yanga zote zipo kwenye mikakati mipya ya kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao, kila upande unaonekana kuwa na maandalizi makubwa kwa kuwa wote watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati maandalizi hayo yakiendelea, habari za ndani ya klabu zinadai kuwa kiungo mkabaji wa Simba Mghana, James Kotei hana nafasi ya kuendelea kuichezea timu hiyo, hali ambayo imesababisha jina lake lianze kutajwa ndani ya Klabu ya Yanga kwa nia ya kumsajili.

Mghana huyo ni kati ya wachezaji waliomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu uliopita na inaelezwa kuwa uongozi wa Simba umepanga kuachana na kiungo huyo mkabaji anayemudu kucheza nafasi zote za ulinzi.

Wachezaji wengine wanaotajwa kuachwa na Simba ni Muivory Coast, Zana Coulibaly, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Mganda Juuko Murshid na Waghana, Asante Kwasi na Nicholas Gyan.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, uongozi wa Yanga upo kwenye majadiliano kwa ajili ya kukamilisha usajili wa kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kukaba.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kuwa wamemfuata kiungo huyo baada ya kupata taarifa za kuachwa na Simba ambayo imemsajili Msudan, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman kwa ajili ya nafasi hiyo ya Kotei.

Mtoa taarifa amefafanua kuwa tayari uongozi wa Yanga unafanya mazungumzo na kocha mkuu wa timu hiyo, Mkongomani, Mwinyi Zahera ambaye kama akipendekeza asajiliwe, basi haraka watakamilisha usajili wake kwa kumfuata nyumbani kwao, Ghana.

“Lipo, wazi Kotei ni kati ya viungo bora katika msimu uliopita wa ligi, tumepata taarifa za kusitishiwa mkataba wake na Simba. “Kiungo huyo tuliwahi kumtaka katika msimu uliopita kabla ya Simba kumuongezea mkataba mpya ambao tayari umemalizika.

“Hivyo, Kotei ni muda wake hivi sasa wa kuja kuichezea Yanga, tumepanga kuwasiliana na kocha kumuelezea mchezaji huyo ambaye anamfahamu na kama akionyesha nia ya kumhitaji, basi tutamsajili,” alisema mtoa tarifa huyo.

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla hivi karibuni alisema: “Uongozi wa Yanga una
uwezo wa kusajili mchezaji yeyote watakayemuhitaji ikiwemo kutoka Simba ilimradi tu kocha amuhitaji.

“Usajili wetu tunaoufanya kwa mujibu wa kocha wetu ambao aliacha majina ya wachezaji anaowahitaji na hivi sasa wanakamilisha kwa kuwasainisha mikataba pekee,” alisema Msolla.

KOTEI HUYU HAPA

Akizungumza na Championi Jumatatu, kutoka kwao Ghana ambapo yupo mapumzikoni Kotei amesema haelewi juu ya hatma yake ndani ya kikosi hicho kutokana na kutopata mawasiliano na kiongozi yeyote wa Simba juu ya kuhitajika kwa msimu ujao.

“Kwa sasa mimi nipo mapumziko tu huku nyumbani, ninacheza na watoto na familia yangu kiujumla sifahamu lolote juu ya usajili wangu.

“Hadi sasa sijapata simu yoyote ile kutoka kwa kiongozi yeyote wa Simba jambo ambalo linanifanya nisielewe juu ya suala la kurudi kwa msimu ujao, labda tuendelee kusubiri kuona inakuwaje hadi siku za mapumziko zitakapoisha,” alisema Kotei.

KUHUSU YANGA

Gazeti hili lilipomuuliza kuhusu kuwaniwa na Yanga na kama yupo tayari kwa ajili ya majukumu yake mapya: “Ninaweza kwenda kokote kule kwa sababu ninataka niwe nacheza tu, siyo Yanga pekee hata klabu nyingine yoyote ile.

“Kama itakuwa hivi kwa Simba kukaa kimya ninaweza kwenda kwingine kokote ambapo mawakala wangu watakuwa wananitafutia. Lakini kitu kikubwa zaidi mimi ninataka kucheza ili nilinde kipaji changu.”

SOMA NA HII  MTIBWA SUGAR YAINYOOSHA KMC JAMHURI, MOROGORO