Home Uncategorized KUSAJILI WAPYA SAWA, LAKINI KWA JAMES KOTEI MTAKOSEA

KUSAJILI WAPYA SAWA, LAKINI KWA JAMES KOTEI MTAKOSEA

Na Saleh Ally
MABINGWA wa soka Tanzania, Simba
wamemchukua mmoja wa viungo bora kabisa
barani Afrika, huyu ni Sharaf Eldin Shiboub Ali
Abdalrahman kutoka nchini Sudan.

Sharaf ni raia wa Sudan ambaye alikuwa
akiichezea Al Hilal, moja ya timu kubwa na
klabu kongwe barani Afrika.

Nilipata nafasi ya kukutana na Sharaf akiwa
kambini, nakumbuka walikuwa wanajiandaa na
mechi dhidi ya watani wao El Merreikh pale jijini
Khartoum.
Nilikwenda hadi pale kwenye uwanja wao
ambako wanaweka kambi. Bahati nzuri kocha
wao Lamine Ndiaye ambaye aliwahi
kuifundisha TP Mazembe alikuwepo na nilipata
nafasi pia ya kuzungumza na Mtanzania,
Thomas Ulimwengu na wachezaji wengine
akiwemo Sharaf.

Siku iliyofuata kwenye uwanja huo,
nikashuhudia mechi kati ya Al Hilal ambao
walishinda dhidi ya Merreikh. Ilikuwa mechi safi
machoni kuitazama, lakini inayoufikirisha
ubongo kutokana na ubora wa wachezaji
wengi. Sharaf alikuwa kati ya walionivutia sana.
Mchezaji huyo ni mtulivu na aina ya uchezaji
wake kwa wale wanaopenda wachezaji
wanaokimbia sana, wanaweza wasivutiwe
naye. Mwendo wake ni wa taratibu kidogo lakini
ni mwepesi kwenye uamuzi wa mambo.
Bora katika utoaji wa pasi zinazofika kwa wakati
mwafaka, lakini anavutia zaidi katika mipira ya
vichwa na anajua aupeleke wapi mpira wakati
mwingine hata anapookoa.
Alichonivutia zaidi, ni namna anavyoweza
kukitumia kifua chake katika mipira mingi kwa
kuwa ni mrefu na bora katika fiziki na hasa
stamina ya miguu.

Kuna Mtanzania mmoja nilizungumza naye
kutoka nchini Sudan baada ya kuona Simba
imemsajili Sharaf. Naye akanieleza kwamba
kweli Simba wamepata “mtu” huku akisisitiza
kuwa wamemsajili kwa kuwa milionea
aliyekuwa akiisaidia timu hiyo amejiondoa
akisema hana fedha baada ya machafuko ya
kisiasa nchini Sudan.
Mtanzania huyo alisisitiza wakati
tukimzungumzia Sharaf: “Kama kungekuwa
kumetulia, Simba wasingeweza kumpata
Sharaf kwa kuwa Al Hilal wasingekubali.
Angalia hata Al Ahly waliwahi kumtaka lakini
ikashindikana, maana ni lulu ya Sudan.”
Nimeanza hivyo nikiamini kuwa Sharaf
ataisaidia sana Simba, hadi yatokee mambo
mengine ya kibinadamu huwezi kujua labda
ashindwe mazingira na kadhalika.
Wakati nafikiria hivyo, kuna kitu niliwaza.
Huenda mambo yatakuwa mengi na vizuri
kuheshimu mapendekezo ya kocha lakini
Simba hawapaswi kumuacha James Kotei
aondoke.
Kotei ndiye mshindani wa Sharaf kwa uhalisia
namba moja lakini kwa wazo la kawaida, au
kwa kutumia moyo ambao hushikilia mapenzi,
basi unaweza kusema Kotei aende tubaki na
Jonas Mkude.
Binafsi Mkude tunaweza kumtetea kama kiungo
Mtanzania au mzalendo lakini ukienda katika
uhalisia, utamkuta Kotei ambaye ana uwezo wa
kucheza zaidi ya nafasi moja.
Namba tatu, sita, tano, wingi ya kulia na
kadhalika. Ni mchezaji ambaye alionyesha
kiwango cha juu zaidi baada ya Simba kupaa
katika hatua za juu zaidi katika Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Utaona kadiri Simba ilivyokuwa inasonga
mbele, kuna wachezaji kadhaa walionekana
kuzidiwa kiuwezo na ilionekana wazi Simba
imepaa katika kiwango ambacho kuna
wachezaji wake wanazidiwa.
Hata Kotei hakuonekana kuwa alikuwa anafaa
sana katika kiwango cha kusema, ni saizi yake
hasa. Lakini kwa sasa, kwa kuwa ameshacheza
katika hatua hiyo, maana yake atakuwa
msaada mkubwa zaidi kwa Simba kuliko msimu
uliopita.
Simba imepata shule kubwa kupitia yeye. Lakini
yeye amejifunza na kuongeza ukomavu ambao
msimu ujao ndio utakuwa una nafasi ya
kuisaidia Simba.
Sijajua kama Simba inamuacha, lakini ninaona
kwa Mkude kusainiwa tena na kuongezwa kwa
Sharaf, maana yake nafasi ya Kotei kubaki
Msimbazi ni ndogo.
Kama itakuwa ataendelea kubaki, ni jambo zuri
kwa Simba kwa kuwa msaada wake utakuwa
mkubwa zaidi. Lakini kama Simba ndio
wanaoona ni sahihi kuachana naye kabisa,
itafika siku nitawakumbusha.
Mchezaji anayecheza nafasi zaidi ya moja, tena
zikafika hadi tatu akiwa anacheza kwa ufasaha,
anakuwa na nafasi mara mbili zaidi ya moja
mnapofikia kuzungumzia usajili. Hivyo
ninaamini kabisa, Simba bado inamuhitaji sana
raia huyo wa Ghana ambaye ni mtu wa shoka
hasa mwenye muonekano wa wembamba wa

reli.
SOMA NA HII  ASEC WATUA NCHINI KUWAKABILI SIMBA