Home Uncategorized WAFAHAMU ZABRON SINGERS, WAIMBAJI WA MKONO WA BWANA WANAOFANANISHWA NA KWETU PAZURI

WAFAHAMU ZABRON SINGERS, WAIMBAJI WA MKONO WA BWANA WANAOFANANISHWA NA KWETU PAZURI

IMEKUWA kawaida kwenye mitandao ya kijamii, hasa kurasa za Instagram ama kwenye makundi ya WhatsApp kusambaza kipande cha wimbo wa  Mkono wa Bwana pindi mambo yanapokuwa tofauti.

Kwa mfano kwa upande wa michezo siku ambayo timu iliyokuwa haijapewa nafasi ya kushinda ikipata matokeo mashabiki wa timu hiyo husambaza kwa kasi kipande cha wimbo huo kujipa moyo.

Wengi wanautambua wimbo na kuwafananisha waimbaji wa wimbo huo sawa na wale walioimba Kwetu Pazuri wenye makazi yao Rwanda ilhali wao ni hapahapa bongo, Mwalimu wao ambaye ni mtunzi pia wa kundi hilo Japhet Zabron anafunguka:-

“Kundi letu linaitwa Zabron Singers kwa sababu wote ni watato wa familia moja, mzee Zabron alikuwa ni kiongozi wetu mkubwa kwenye ukoo wetu hivyo tukaamua kuendelea kumuenzi.

“Sote tunaimba tukitoka kwenye mashina yetu wenyewe hivyo hili kundi limeanzishwa ndani ya familia hali inayofanya iwe ngumu kutengeneza matabaka ndani ya kundi letu.

Kundi lina waimbaji wangapi?

“Kundi letu lina jumla ya waimbaji 15 ambao tunafanya nao kazi kwa kushirikiana ila bado tuna amini litakuwa kubwa hapo baadaye kwa kuwa ukoo wetu ni mkubwa.

“Tumeanza kuongeza pia kwa kuwafundisha wengine ambao wapo nje ya Zabron pia kupitia kujitoa kwetu kwa jamii hii inafanya tuwe ni familia kubwa bila kujali dini wala kabila.

Kundi limeanzishwa lini?

“kundi letu limeanzishwa mwaka 2006 makao makuu ni mkoa wa Shinyanga, wilayani Kahama tupo chini ya kanisa la wasabato linaitwa Kahama Central SDA na mlezi wetu ni Benedict Burash.

Kwa nini mliamua kuandika Mkono wa Bwana?

“Mengi ambayo Bwana alikuwa anatundea nyuma hata sasa amekuwa akitutendea ni mkono wake hali iliyofanya tukaandika huo wimbo.

“Ilikuwa ni wakati ambao tunaongea na Bwana na kutaka aongee na watu wake wote bila kujali aina ya dini, kabila wala rangi ndipo tukauona Mkono wa Bwana.

Je Mkono wa Bwana mmeuona kweli?

“Hakika mkono wa Bwana tumeuona, namna ambavyo tumegusa hisia za mashabiki na kubadilisha mienendo yao inabadilika na kutenda matendo mema hivyo kwetu ni faraja na tunaamini wengi wanauona mkono.

Kundi lina albamu ngapi?

“Kwa sasa tuna jumla ya albamu tatu ambapo albamu yetu ya kwanza inaitwa Nawakumbuka ilitoka mwaka 2012 ina jumla ya nyimbo 11, albamu ya pili inaitwa Mkono wa Bwana mwaka 2015 na albamu ya tatu inaitwa Sio Bure ina nyimbo 9 imetoka mwaka 2018.

Kwa nini mkono wa Bwana imepokelewa vizuri mwaka 2016?

“Wakati wa Bwana ukifika hakuna anayeweza kuuzuia, tulitunga wimbo mwaka 2013 tukarekodi mwaka 2014 tukauachia mwaka 2015 ukaja kupokelewa vizuri 2016 na mpaka leo bado unaskilizwa na kupendwa.

“Tulimwomba Mungu aweze kutushika mkono na akatuonyesha njia mpaka tukafanikiwa kuandika nyimbo hii, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa wengi walikuwa hawaamini kama tunaweza kufanya kitu kikubwa kulingana na jinsi tulivyo na ndio maana mpaka sasa wimbo ni mkubwa kuliko sisi tulivyo.

Ugumu ulikuwa wapi kufanikisha mliyoyafanya?

“Kukubalika na kupewa nafasi, mengi yalikuwa magumu kwetu kwani hatukuwa tukipewa muda wa kusikilizwa kazi zetu, ni mapito ambayo tumeyapitia na kikubwa tuliamini kwamba ni lazima tuuone mkono wa Bwana na imetokea.

Kipi ambacho mnamshukuru Mungu?

“Katika kila jambo ambalo tunapitia tunamshukuru Mungu, namna ambavyo injili yetu inafika ulimwenguni kote pamoja na kukubalika katika jamii tunasema asante.

Malengo ya kundi kwa sasa ni yapi?

“Kumtumikia Mungu na kufanya kazi nyingine bora zaidi ya mkono wa Bwana na ndio maana kwa sasa tupo kwenye mpango wa kutengeneza albamu ya nne ambayo itakuwa ni moto wa kuotea mbali zaidi ya Mkono wa Bwana.

“Kufanya Zabron iwe taasisi kubwa ya kusaidia jamii na kuinua vipaji vya wengi ambao wamekata tamaa ili kuendelea kupambana.

“Kufanya kazi na wasanii wengine nje ya kundi letu ili kuendeleza huduma na kuwafikia watu wengi zaidi.

Matokeo ya Mkono wa Bwana ni nini?

“Katika hili hakika tumeuona mkono wa Bwana kwani tumekuwa tukipata mialiko mbalimbali mikubwa na midogo, ndani na nje ya nchi.

“Tumefanikiwa kufika Uganda, Kenya na kufanya matamasha, pia tuna amini tutauona mkono wa Bwana tutaipeleka Ulaya kufanya matamasha.

Gharama za studio mwanzo ilikuaje?

“Mwanzo tulikuwa tunachangiwa na Hamis Bukuru ila kwa sasa tayari tumeshakuwa na uwezo wa kumudu gharama, ambapo kupitia kazi zetu kwenye mitandao ya kijamii kama youtube chaneli pamoja na matamasha tunapata fedha za kuendeleza kazi zetu.

Unawaambiaje mashabiki?

“Kazi ya Bwana yatupasa tuitende kwa moyo hivyo sapoti yao ni jambo la msingi kila siku na ndio maana tunafanya kwa ajili yao hivyo wakati wa Bwana ni siku zote, kama ambavyo nasi tulikuwa na subira mpaka muda wa Bwana ulipofika nao pia wanapaswa wawe na subira kutafuta mafanikio,” anamaliza Zabron. 

SOMA NA HII  HESABU ZA MTIBWA SUGAR ZIPO NAMNA HII