Home Uncategorized YANGA HII NI JEURI, MILIONI 930 KUSAJILI JEMBE

YANGA HII NI JEURI, MILIONI 930 KUSAJILI JEMBE


YANGA kwa sasa wana jeuri ya kumsajili mchezaji yeyote wamtakaye kutokana na kuwa na kitita cha Sh milioni 930 ambazo wamezipata katika harambee yao ya Kubwa Kuliko.

Kwa wiki kadhaa nyuma, Yanga wamekuwa wakichangia fedha kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo ambapo Jumamosi iliyopita walifikia tamati zoezi hilo katika harambee kubwa iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amesema baada ya michango yote kukamilika, wamefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha kutoka kwa wanachama wao ambazo watazielekeza kwenye masuala ya usajili.

“Tulikuwa na suala la michango kwa klabu yetu katika kusaidia baadhi ya mambo mbalimbali ambapo Jumamosi ya Juni 15 tulihitimisha zoezi letu ambalo wanachama walikuwa wakituma fedha kwa njia mbalimbali.

“Tunawashukuru watu wote waliochangia na tumekusanya kiasi cha Sh milioni 930, fedha ambazo zitaenda kufanya mambo ya uendeshaji wa klabu lakini pia suala la usajili. Bado tunatoa wito kwa wanachama wetu kuendelea kuchanga.

“Nje ya hilo, Julai 27 tutakuwa na kilele cha Wiki ya Mwananchi ambayo itafanyika wiki nzima ambapo tutakuwa tunafanya huduma za kijamii na mwisho siku hiyo tutatambulisha wachezaji wetu wapya na tutacheza mechi moja ya kirafiki na timu moja mashuhuri ambayo tunaendelea kuongea nayo, kauli mbiu katika wiki hiyo ni Funga Kazi, Kusanya Kijiji,” alisema Mwakalebela.

KAMBI MAPEMA

Mwakalebela aliongeza kwamba kikosi hicho kitaingia kambini Julai 7, kwa ajili ya kuanza maandalizi yake ya msimu ujao. “Kambi tutaianza Julai 7, ambapo tunaweza kwenda kuweka sehemu nyingine tofauti na hapa.”

SOMA NA HII  HOTEL YA KITALII YA SNOWCREST ARUSHA YADAIWA KUFILISIWA