Home Uncategorized EXCLUSIVE: KAHATA RASMI ASAINI SIMBA, AKOMBA SH MIL. 80

EXCLUSIVE: KAHATA RASMI ASAINI SIMBA, AKOMBA SH MIL. 80


RASMI kiungo mchezeshaji wa Timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars na Klabu ya Gor Mahia, Francis Kahata ni mali ya Simba baada ya kufikia makubaliano ya kusaini mkataba kwa dau la shilingi milioni 80 akiwa nchini Misri.

Kahata aliyepo nchini Misri kwenye michuano ya Afcon, anajiunga na Simba akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika ndani ya Gor Mahia.

Kiungo huyo fundi anasaini mkataba huo wa kujiunga na Simba akichukua nafasi ya Mnyarwanda, Haruna Niyonzima aliyeaga mashabiki wa timu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika.

Habari kutoka ndani ya kambi ya Harambee nchini Misri ni kwamba kiungo huyo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu.

Taarifa zinasema kuwa, Kahata atakuwa analipwa shilingi milioni 8 kila mwezi katika kipindi cha miaka mitatu atakachokuwepo Simba.

Habari zinasema kwamba kiungo huyo amemalizana na viongozi wa Simba kwenye kambi ya Harambee nchini Misri na akitoka huko ataunga moja kwa moja kwenye kambi ya Simba.

“Kahata atakutana tena na kucheza pamoja na rafiki yake kipenzi Meddie (Kagere) waliokuwa wanacheza wote hapa Gor Mahia,” kilisema chanzo chetu ndani ya kambi hiyo. Mwekezaji wa Simba Bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’ hivi karibu alisema kuwa kuwa:

“Simba imejipanga vema kwa ajili ya msimu ujao na kikubwa tunaahidi kufanya usajili bab kubwa kwa gharama yoyote ndani ya Ukanda wa Afrika.

“Kikubwa tunataka kuona Simba ikipata mafanikio kama ilivyokuwa Zamalek, Al Ahly na TP Mazembe ambazo zimechukua mataji makubwa Afrika.” Jana Jumanne, magazeti mbalimbali nchini Kenya yaliuhabarisha umma juu ya usajili huo wa Kahata kujiunga na Simba.

SOMA NA HII  MCHEZO MZIMA WA SIMBA KUMALIZANA NA BIASHARA UNITED KWA 4G ULIKUWA HIVI