Home Uncategorized JESHI KAMILI LA YANGA HILI HAPA, SALAAM ZAO WAPINZANI

JESHI KAMILI LA YANGA HILI HAPA, SALAAM ZAO WAPINZANI


YANGA ndiyo timu pekee iliyofanya usajili wa haraka na kukamilika kabla dirisha la usajili kufunguliwa rasmi jana.

Dirisha hilo la usajili linatarajiwa kufungwa Julai 31, mwaka huu na hakutakuwa na muda wa kuongezwa huku usajili wa Caf kwa klabu za Simba, Yanga, Azam FC na KMC ukitarajiwa kufungwa Julai 10.

Yanga na Simba zinatarajiwa kuiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam na KMC zenyewe zikiwakilisha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika usajili wao mpya, Yanga imefanikiwa kusajili nyota wapya 13 huku ikiwa imewaboreshea mikataba wachezaji wake waliomaliza kwa mujibu wa mapendekezo ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani, Mwinyi Zahera.

Kwa usajili uliofanywa, kikosi cha Yanga katika msimu ujao kitakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na idadi kubwa ya wachezaji wapya waliosajiliwa na kusababisha timu hiyo kuingia mapema kambini kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi.

Yanga, imepanga kuanza maandalizi ya msimu ujao kwa kuanza kuweka kambi jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda nchini China itakapokwenda kuweka kambi hiyo.

Wachezaji wote waliosajiliwa na Yanga kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kuanza kutua nchini kuanzia wiki hii kwa ajili ya kambi hiyo inayotarajiwa kuanza Julai 7 , mwaka huu itakayokuwa chini cha Kocha Msaidizi Mzambia, Noel Mwandila huku akimsubiria Mwinyi Zahera aliyeko Misri kwenye Afcon.

Usajili huo kamili wa Yanga ni huu ambao makipa ni watatu nao; Farouk Shikhalo (Mkenya), Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili. Mabeki wa pembeni ni Ally Sonso, Gadiel Michael (bado ana mvutano na Yanga lakini anatarajiwa kusaini), Paul Godfrey na Juma Abdul.

Mabeki wa kati ni Mustafa Suleiman (Burundi), Kelvin Yondani, Lamine Moro (Mghana), Andrew Vicent ‘Dante’, Ally Ally na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Viungo ni Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Papy Tshishimbi (DR Congo), Mohamed Issa ‘Banka’, Raphael Daud, Mapinduzi Balama, Patrick Sibomana (Rwanda), Deus Kaseke na Mrisho Ngassa ‘Anko’.

Washambuliaji ni Juma Balinya (Uganda), Maybin Kalengo (Zambia), Issa Bigirimana (Rwanda) na Sadney Urikhob (Namibia) ambao wote kutoka nje ya nchi na Juma Mahadhi aliyependekezwa kubakishwa na kocha Zahera.

Akizungumzia hilo, mwenyekiti wa timu hiyo, Dr Mshindo Msolla alisema usajili wao kwa asilimia 90 umekamilika.

“Tumesajili wachezaji 27, tumebakiza nafasi tatu kwa ajili ya dharura, hasa kama kocha atahitaji wachezaji wengine katika usajili wa dirisha dogo,” alisema Msolla.

SOMA NA HII  MTIBWA SUGAR: MUHIMU KUCHUKUA TAHADHARI YA VIRUSI VYA CORONA