Home Uncategorized KAHATA AANZA NA MIKWARA SIMBA

KAHATA AANZA NA MIKWARA SIMBA


Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, kiungo mchezeshaji wa Simba raia wa Kenya, Francis Kahata, ametamba kuwa anakuja Msimbazi kucheza na siyo kukaa benchi.

Kauli hiyo huenda ikawa tishio kwa wachezaji wanaocheza naye nafasi moja (namba nane) ambao msimu uliopita walikuwa wakibadilishana kucheza Mzambia, Clatous Chama, Hassani Dilunga, Mzamiru Yassin na Jonas Mkude kabla ya Msudan wa Al Hilal, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman kusaini hivi karibuni.

Kahata amesaini kuichezea Simba kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika Gor Mahia aliyokuwa anaichezea kabla ya kuja kusaini Msimbazi iliyokuwa inawania saini yake kwa muda mrefu.

Kahata alisema hatima yake ya kucheza au kutocheza ipo mikononi mwa Kocha Mkuu Mbelgiji, Patrick Aussems lakini kikubwa amekuja Simba ili kuhakikisha anaingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Kahata alisema kuwa hakuna mtu wa soka asiyefahamu uwezo wake wakiwemo viongozi, mashabiki na kocha wa timu hiyo aliyependekeza usajili wake.

Aliongeza kuwa, anaheshimu uwezo wa kila mchezaji ndani ya Simba, wakiwemo wapya na wa zamani huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa timu hiyo.

“Mimi siku zote ninapenda ushindani kwenye kila klabu yangu mpya nitakayokwenda kuichezea, kwa maana kucheza katika kikosi cha kwanza na hicho ndiyo kitu cha kwanza.

“Lakini ninaahidi kupambana kwa kuhakikisha ninatimiza majukumu yangu ya ndani ya uwanja ikiwemo kuchezesha timu, kutengeneza nafasi za kufunga mabao, pia mimi mwenyewe kufunga.

“Ninafahamu nina majukumu makubwa ndani ya Simba, ni baada ya kujiunga nayo na kati ya hayo ni kuhakikisha tunachukua makombe yote tutakayoshiriki katika msimu huu,” alisema Kahata.

Katika hatua nyingine, mshambuliaji wa timu hiyo Mnyarwanda, Meddie Kagere amemkaribisha Kahata aliyekuwa anacheza naye pamoja Gor Mahia kwa kumwambia: “Karibu Simba rafiki yangu Kahata kwenye changamoto mpya ya ushindani na jisikie upo nyumbani.”

SOMA NA HII  BEKI HUYU WA UGANDA ATAJWA KUWA KWENYE RADA ZA YANGA