Home Uncategorized OKWI ATAKA 115M KWA MWAKA SIMBA

OKWI ATAKA 115M KWA MWAKA SIMBA


STRAIKA wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi ameyaamsha tena mambo ndani ya klabu yake hiyo baada ya kuwaambia viongozi kwamba kama wanataka asalie klabuni hapo, basi wamuwekee benki kitita cha Sh milioni 115 kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Okwi aliye nchini Misri kwenye Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), amemaliza mkataba na Simba ambapo wanavutana na uongozi wa klabu hiyo juu ya kusaini mkataba mpya.

Siku chache nyuma uongozi wa Simba, ulidaiwa kukutana na Okwi huko nchini Misri na kuzungumza naye juu ya mkataba mpya ambapo bado mambo ni moto.

Mpaka kufikia juzi jioni Okwi anadaiwa kuendelea na msimamo wake wa kutaka apewe mkataba wa mwaka mmoja kwa kitita cha Sh milioni 115 badala ya kusaini miaka miwili kwa kitita hicho ambacho uongozi wa timu hiyo unataka umpatie.

Habari za kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatatu, limezipata zimedai kuwa msimamo huo wa Okwi unaendelea kuwatesa viongozi hao wa Simba.

“Bado Okwi kasimamia msimamo wake wa kutaka apewe mwaka mmoja kwa kitita cha Sh 115 milioni kama kweli uongozi unataka abakie katika kikosi chetu.

“Lakini uongozi wenyewe unataka kumpatia fedha hizo ila asaini miaka miwili jambo ambalo Okwi halitaki, kwa hiyo kumekuwa na mvutano juu ya hilo.

“Mpaka sasa licha ya uongozi kutumia watu mbalimbali kumshawishi ili asaini mkataba mpya, bado kasimamia msimamo wake huo huku akidai kuwa kama wanataka asaini miaka miwili basi waongeze fedha,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Okwi hakuweza kupatikana huku ikidaiwa kwamba amebadilisha namba yake anayotumia.

Lakini pia hali hiyo ilijitokeza kwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori ambaye pia alipotafutwa ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana.

SOMA NA HII  REKODI ZA JEMBE JIPYA YANGA USIPIME, KESHO NDANI YA CHAMPIONI JUMATANO