Home Uncategorized KUMBUKENI KILA MLICHOFANYA HAKITAZUIA NYIE KUPOTEZA MICHEZO

KUMBUKENI KILA MLICHOFANYA HAKITAZUIA NYIE KUPOTEZA MICHEZO


NA SALEH ALLY
UKITAKA ujifunze mambo mengi, wakati mwingine ni vizuri sana kujiuliza maswali ya kutosha na kutafuta majibu sahihi ya kutosha kuhusiana na kile ambacho unakipenda.

Mpira ndio mchezo unaopendwa kuliko mingine yote duniani. Je, umewahi kujiuliza kwa nini? Angalau hata kama kuna majibu 10 sahihi, basi wewe ukapata hata matano ambayo yatakuwezesha kujua unachokipenda kina nguvu ipi au ndani yake kuna nini.

Najua, wengi hatupendi kusumbua vichwa vyetu kwa vitu ambavyo tunaona havina maana lakini leo nataka nikuambie mambo baadhi.

Soka kuonekana kuwa mchezo ambao haujali wenye fedha au masikini, imesaidia sana kujiongezea watu wengi kuufurahia na kuupenda sana na hasa katika mabara ya Amerika Kusini, Afrika na Asia.

Kwingine umekuwa kama shule na wanapata vifaa sahihi muda wote wa kujifunza soka. Lakini bado nyota wengi sana wanatokea katika mabara matatu ambayo nimeanza kuyataja.

Pamoja na mengi ambayo unaweza kujifunza, moja ya kitu cha ndani kimeufanya mchezo wa soka kupendwa zaidi ni kutotabirika kirahisi.

Watu wengi hawapendi majibu rahisi au kitu kinachojulikana moja kwa moja majibu yake yatakuwa yapi.

Mchezo wa soka, hautoi nafasi ya kupata jibu rahisi au la moja kwa moja kuwa tu upande mmoja una fedha nyingi, una wachezaji wengi kutoka Ulaya au una kocha bora zaidi.

Mchezo huu una majibu yasiyoeleweka na ndio maana kocha wa zamani wa Chelsea na Manchester United, Jose Mourinho amekuwa akisema mchezo wa soka una matokeo ya kikatili sana.

Hii inatokana na namna ambavyo amekuwa akipitia, inawezekana amekutana na timu ambayo anaamini haina uwezo kabisa wa kuifunga timu yake kutokana na ubora wake kama kocha na kiwango cha wachezaji alionao lakini mbele ya mashabiki wao ambao wanawaamini. Mwisho yeye anaishi kufungwa.

Anachokisema Mourinho kimewakuta wengi sana na siku moja ubaya ukawa kwao, siku nyingine ubaya ukawa kwa wengine lakini siku nyingine furaha ikawa kwake na wakati mwingine ikawaangukia wengine.

Hii ni sehemu kubwa ya kuufanya mchezo wa soka kuwa kipenzi cha wengi. Hauna majibu sahihi kiulaini, hauonei mtu na unatoa nafasi kwa kila mtu kujionea au kujipendelea mwenyewe, utachagua.

Kupitia hii, inakuwa vizuri sana kwa mashabiki wa soka nyumbani kujikumbusha kabla ya msimu wa Ligi Kuu Bara haujapamba moto. Najua umeanza, lakini imekuwa kimyakimya sana kwa kuwa vigogo wote watatu hawajacheza hata mechi moja kwa kuwa wako katika mashindano ya kimataifa.

Simba waliweka kambi Afrika Kusini, hii haiwapi uhakika lazima washinde kila mchezo na wanaweza kupoteza mchezo hata dhidi ya Ndanda FC ambayo haikuwa na kambi bora.

Kila kitu katika soka kina mwendelezo. Baada ya kambi mnatakiwa kuendelea kujiimarisha kwa mchezaji mmojammoja na mwisho kikosi kizima. Katika mechi lazima msimamie ubora kwa kuwa dakika 90 zinajitegemea, ukikosea unaadhibiwa.

Yanga ambayo ilikuwa na kambi nzuri Morogoro, inaweza kufungwa na Mwadui FC ambayo huenda kambi haikuwa bora sana. Lakini hata Azam FC pamoja na wachezaji wengi wapya, bora, kocha mzuri, pia inaweza kupoteza dhidi ya Biashara FC ambayo inawezekana haikuwa imeshinda mechi hata moja.

Angalia Yanga iliyokuwa Morogoro, imeing’oa Township Rollers kwao Botswana kwa kuipa kipigo cha 1-0 wakati timu hiyo ilipiga kambi takribani mwezi mzima nchini Afrika Kusini na kuacha mamilioni kule.

Hivyo mchezo wa mpira, hautoi nafasi kuwa kambi nzuri basi wewe utashinda tu. Una washambulizi wa kati au viungo maarufu basi hautafungika. Siku ikifika ukakosea, utafungwa tu na hivyo inakuwa chachu ya wewe kujipanga upya na kulenga kufanya vizuri tena.

Maana yangu ni hivi, siku ikitokea timu imepoteza hasa kwa Yanga na Simba, isionekane kuna mchawi na kusababisha migogoro. Huu ndio mchezo wa soka.

SOMA NA HII  LIGI KUU BARA KUENDELEA LEO, HIZI HAPA KUMENYANA MKWAKWANI