Home Uncategorized NYOTA YANGA AMKOSESHA AMANI KIPA TOWNSHIP ROLLERS

NYOTA YANGA AMKOSESHA AMANI KIPA TOWNSHIP ROLLERS


KIPA tegemeo wa Township Rollers, Wagarre Dikago amekiri kutoka moyoni kwamba kuna mchezaji mmoja tu anamnyima usingiza ndani ya Yanga ambaye ni Patrick Sibomana.

Straika huyo raia wa Rwanda ndiye aliyefunga bao pekee la Yanga kwa mkwaju wa penalti huku akikosa mwingine hapo awali na aliingia kwenye boksi mara nyingi.

Dikago ameliambia Spoti Xtra linaloongoza kwa mauzo kila Alhamisi na Jumapili kwamba, kila mara mazoezini anafanya mbinu za jinsi ya kumkabili Sibomana ambaye alimtesa sana kwenye mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 Jijini Dar es Salaam, wikiendi iliyopita. Dikago amesema kwamba Sibomana asipokuwa nae makini ataumaliza mchezo wa marudiano Agosti 24 kirahisi.

“Yule jamaa aliyepiga penalti ile alinipa wakati mgumu sana na alikuwa anatumia zaidi mguu wa kushoto. “Ana uwezo na nguvu, huyu jamaa ni hatari sana, ninamfanyia kazi ya ziada sana kumkabili anajua mbinu za mpira. “Hata ukiangalia mashuti yake yalinipa wakati mgumu sana haswa ile penalti ya bao,” alisema kipa huyo mwenye kigugumizi.

Alisisitiza kwamba mchezo wa marudiano utakuwa vita kubwa na hawatakubali kupoteza mbele ya Yanga. Kocha Mwinyi Zahera ametamka kwamba mechi mbili watakazocheza dhidi ya Polisi Tanzania na AFC Leopards ya Kenya zitakuwa na mkakati maalum na itachezwa kwa staili maalum.

Alisema kwamba watazipa timu hizo hata fedha zifanye mazoezi ya staili ya Township na kucheza kwa staili hiyo ili kuwarahisishia mechi yao ya ugenini.



SIKU 76 ZA SIBOMANA Kesho Ijumaa Yanga itajipima na Polisi Tanzania katika mchezo wa kirafiki, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi. Kabla ya mchezo huo, jana Jumatano Sibomana alitimiza siku 76 tangu alipomwaga wino Jangwani. Sibomana ambaye amejiunga na Yanga akitokea Mukura FC ya nchini Rwanda, ameandika rekodi kabambe ya kuzifumania nyavu.

Sibomana anaongoza kwa kuzifumania nyavu kwa sasa katika kikosi cha Yanga kuliko wachezaji wengine wote. Katika mechi tisa za kirafiki pamoja na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo Yanga imecheza mpaka sasa, Sibomana ameifungia timu hiyo mabao nane akifuatiwa na Juma Balinya ambaye yeye amezifumania nyavu mara tano.

Mechi hizo ni zile ambazo Yanga ilicheza ilipokuwa kambini mkoani Morogoro ambako ilicheza mechi sita lakini pia ile kimataifa dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya.

Mechi dhidi ya Mlandege na Malindi zote za Zanzibar pamoja na ile ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Township Rollers ya Botswana. Akizungumza na Spoti Xtra kuhusina na rekodi hiyo, Sibomana alisema kuwa: “Mipango yangu ni kuhakikisha nafanya vizuri zaidi ili niweze kuisadia timu yangu kufanya vizuri msimu huu. Siangalii rekodi ila ninachoangalia ni kuisaidia timu yangu.”

CHUO CHA WANYAMA

Yanga ambayo juzi Jumanne ilitua Moshi mkoani Kilimanjaro, inafanya mazoezi katika Chuo cha Mwika Wildlife kilichopo eneo la Kibosho.

Chuo hicho kinajihusisha na masuala ya wanyama ambapo eneo hilo wapo wale wanyama ambao siyo wakali. Ni sehemu sahihi kwao kutokana na maagizo ya Kocha Mwinyi Zahera aliyetaka kambi yenye baridi sana kwani hapo ni karibu na Mlima Kilimanjaro, hivyo suala la baridi si la kuuliza.

SOMA NA HII  ISHU YA MASHABIKI WA SIMBA KUPIGWA JANA, YANGA WATOA TAMKO