Home Uncategorized SUALA LA OKWI LAIBUKA UPYA SIMBA, KIGOGO AFUNGUKA JUU MATUMIZI YA FEDHA...

SUALA LA OKWI LAIBUKA UPYA SIMBA, KIGOGO AFUNGUKA JUU MATUMIZI YA FEDHA ZAKE


Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba na shahidi namba nane katika kesi inayowakabili waliokuwa viongozi Simba, Kassim Dewji ameieleza mahakama jinsi walivyopanga matumizi ya fedha za mauzo ya mchezaji  Emmanuel Okwi ambaye alikuwa ameuzwa nchini Tunisia.

Ushahidi huo, ulitolewa kwenye kesi ambayo inawakabili waliokuwa viongozi wa Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange (Kaburu) pamoja na mwenyekiti  wa kamati ya usajili, Zacharia Hans Pope.

Kassim ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya michezo vya Kampuni ya Romario Sports 2010 Limited, aliiambia  mahakama akiwa mjumbe wa kamati ya utendaji chini ya uongozi wa Evans Aveva waliitwa kamati ya utendaji na kuelezewa kuwa fedha ambazo aliuzwa mchezaji Okwi kwenye Klabu ya Etoile du Sahel, dola 300,000 zimefika.

Shahidi huyo aliielezea mahakama kuwa kamati ya utendaji walijadiliana matumizi ya zile fedha. “Kipindi tunajadiliana kuhusu zile fedha dola 300,000 Simba ilikuwa na madeni mengi na mengine ya nyuma ya uongozi uliopita.

“Tukaona zile fedha zinaweza kuisha, kuna mwenzetu mmoja tulikuwa tumekopa ambaye ni Hans Pope tuliamua kumlipa fedha yake ambayo ilikuwa ni dola 17,000.

“Baada ya hapo fedha ambayo ilibakia kama kamati tulikubaliana kuwa ifunguliwe akaunti ambayo zile fedha zitaweka na ni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Bunju ambapo hapo kulitakiwa manunuzi ya nyasi bandia kumlipa mkandarasi na mambo mengine.

“Na hiyo akaunti aliyetakiwa kuifungua ni rais (Aveva) pamoja na mhasibu/katibu (Amos), ndiyo walikuwa na jukumu hilo kwa kuwa ndiyo watendaji wa juu.

Pia iliundwa kamati ya kusimamia uwanja huo iliitwa Bunju Project, lakini baada ya hapo sikujua kama akaunti ilifunguliwa au la sababu sikuhudhuria tena kwenye kikao cha kamati ya utendaji kwa kuwa nilisafiri,” alisema Kassim.

Baada ya ushahidi huo, kesi hiyo ambayo ipo chini ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba aliahirisha mpaka Septemba 4, mwaka huu.

SOMA NA HII  HUU HAPA MTAMBO WA KUTENGENEZA MABAO NDANI YA MANCHESTER CITY