Home Uncategorized KASEJA TUNAMSIFIA LAKINI TUKUMBUKE TULIPOMTENGA ILI TUSIRUDIE KWA WENGINE

KASEJA TUNAMSIFIA LAKINI TUKUMBUKE TULIPOMTENGA ILI TUSIRUDIE KWA WENGINE



NA SALEH ALLY
KAMA itakuwa ni ishu ya maswali basi tutasema mjadala umefungwa kwa kuwa hakuna cha kuuliza tena.
Pamoja na hivyo unaweza kujiuliza namna gani Kaseja leo ni shujaa mkubwa wa timu ya taifa baada ya miaka mingi ya kuonekana amekwisha na matatizo makubwa.

Jiulize nani aliyemuinua Kaseja baada ya kuangushwa kwa nguvu, ni mkewe au rafiki zake? Ni wana familia au majirani zake? Hata kama hatuwajui lakini ukweli uko hadharani leo kwamba Kaseja ni shujaa wa taifa, shujaa ambaye alilifanyia taifa mambo makubwa, mwaka 2003, wengine ambao hawakuwa wameanza hata shule ya msingi na leo wana familia.

Jana, Kaseja ameibuka shujaa tena kwa kufanikiwa kuokoa penalti huku akikaa imara langoni wakati Taifa Stars ikiitwanga Burundi kwa mabao 3-0 ya mikwaju ya penalti na kusonga mbele.

Mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya bao 1-1 nchini Burundi na jana Warundi wakakomaa na kupata sare ya 1-1, hivyo kufanya ziongezwe dakika 30 ambazo hata hivyo hazikuwa msaada kwao na badala yake kwa Tanzania na Kaseja amekuwa shujaa tena.

Kabla ya mechi ya Burundi, Kaseja alikuwa shujaa pia akiisaidia Stars kusonga mbele kwenye michuano ya Chan dhidi ya Kenya. Huyu ni Juma Kaseja, Mtanzania ambaye mlimkatisha tamaa kwa nguvu kwa hamu na matakwa yenu binafsi, leo ukweli unawasuta.

Nawaasa viongozi wa klabu, husda haiwezi kuwa msaada katika mpira wetu, msiingize mambo binafsi na kuchanganya na kazi na mwisho kulazimisha kuua vipaji vya watu tukiwaaminisha hawana uwezo.

Mliomdhulumu Kaseja, leo msimame na kusema mlichoiaminisha jamii hakikuwa sahihi. Najua mnaweza kushindwa kufanya hivyo, lakini leo nafsi zenu zinaumizwa na uongo, unafiki na uzandiki wenu. 

Si ajabu ukasikia siku moja Kaseja amerejea Simba kwa kuwa kiwango chake baada ya kucheza ligi kuu zaidi ya miaka 10, kinaonyesha ni cha juu kabisa. Hongera Kaseja, hongera moyo wako kwa kusimama imara mbele ya wababaishaji waliolazimisha “kukua”.

Naachana na Kaseja, narejesha nguvu kwa kikosi cha Taifa Stars baada ya mechi ya jana ambayo hakika niliiangalia kwa utulivu mkubwa.

Hakika vijana wetu wamepambana katika kila idara na walifanya kazi kubwa sana kuhakikisha tunafanikiwa kusonga mbele.

Kuna wakati vijana wetu walionekana kukosa mbinu za kujikwamua. Lakini mapambano yao yalionekana ni wale waliokuwa wakijua kuna watu walio nyuma yao na wasingetaka kuwaangusha.

Kazi mmefanya kubwa sana, kazi ya kiume na mapambano ya kijeshi na mnastahili sifa iliyotukuka kwamba mmefanikiwa kuipeleka Stars katika hatua ya makundi kuwania kucheza Kombe la Dunia mwaka 2022, nchini Qatar.
Kwa wale ambao hata wamewahi kucheza soka la cha ndimu, wanajua haikuwa kazi nyepesi na Burundi walijiandaa hasa kwa ajili ya mechi hiyo ngumu lakini mwisho, furaha tumebaki nayo sisi.
Waliosababisha tubaki na furaha ni wachezaji lakini makocha au benchi la ufundi kwa ujumla pamoja na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao kwa kuwa hili ni jukumu lao na hasa maandalizi, hakika walifanya mambo ya uhakika kufanikisha hilo.
Hongera kwenu nyote ambao mnajua mmeshiriki lakini hongera nyingi zaidi ziende kwa mashabiki mliofika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwamba hamasa yenu, kelele na “hamasisho sisitizo” kwa wachezaji wetu limechangia kuamsha morali kuu.
Mnastahili pongezi kwa kiwango cha juu na muamko huu, unapaswa kuendelea tena na tena kila Taifa Stars inapokuwa uwanjani. Mungu Ibariki Tanzania.



SOMA NA HII  NORWICH YAIKAZIA LIVERPOOL KWA LEWIS