Home Uncategorized TWENDENI TAIFA TUKAWAPIGE PAMOJA BURUNDI TWENDE KOMBE LA DUNIA

TWENDENI TAIFA TUKAWAPIGE PAMOJA BURUNDI TWENDE KOMBE LA DUNIA



NA SALEH ALLY
UTAIFA hauwezi kuwa nyimbo za mdomoni pekee, badala yake vitendo vinavyothibitisha nia na hamu ya utaifa wa mtu.

Moja ya nguzo ya utaifa ni ushiriki wa mambo ya utaifa kwa nia njema na taifa lako. Kusaidia mambo ya msingi kwa faida ya taifa lako ni utaifa hasa, na wakati umefika wa kulidhihirisha hilo.

Timu ya taifa ya soka ya wasichana chini ya miaka 17, itashuka dimbani Jumapili hii kuwavaa Burundi katika mechi yao ya kwanza.

Mechi hii itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na vijana hao wanatakiwa kushinda au kufanya vizuri ndani ya mechi sita tu ili wafanikiwe kucheza Kombe la Dunia, michuano itakayofanyika nchini India kati ya Novemba 2 hadi 21, mwaka huu.

Nimesema mechi sita kwa kuwa watacheza na timu tatu hadi wanafuzu lakini mechi zitakuwa nyumbani na ugenini. Kama mechi ya Jumapili wanaanzia nyumbani na baada ya hapo watasafiri hadi Bujumbura kwenda kuwavaa Burundi wakiwa kwao.

Kwa kuangalia, unaweza kuona ni kama kazi nyepesi kutokana na uchache wa mechi lakini uhalisia, mambo si rahisi kwa kuwa kuna timu bora ambazo lazima wakutane nazo na zitakuwa na upinzani mkubwa.

Kwa Watanzania hata kama tutakuwa wengi kiasi gani hatuwezi kuingia uwanjani na kucheza kwa kuwa kuna kanuni za Fifa lakini bado tuna nafasi kubwa ya kuwa wataifa au wazalendo na msaada wetu ukafikia kwa dada na wadogo zetu hao wakiwa wanapambana kwa ajili ya taifa letu.

Ni kitu kimoja tu hapo, kwenda uwanjani kwa wingi kwa ajili ya kazi ya kushangilia kwa nguvu na kuwaonyesha kweli tuko pale kwa ajili yao, tumekwenda pale kuwapigania na kuwaunga mkono.

Tunatakiwa pale kuwaonyesha kuwa sisi Watanzania tunatambua umuhimu wa timu yetu ya taifa kucheza Kombe la Dunia. Hakika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likijitahidi sana kuziandaa timu zetu za kinadada au wanawake.

Ninatambua ni gharama lakini kuna matunda tumeyaona na kwa sasa kila sehemu duniani kote wameweka nguvu katika soka la wanawake kwa kuwa vipaji vya wanawake vimeanza kuuteka ulimwengu wa soka.

Mfano kwa nchi za Afrika, kama Algeria na Misri kwa sasa wamekuwa na kiwango cha juu sana katika soka la wanawake baada ya kuona kuna kitu na wanastahili kukiongezea nguvu. Sasa wameweka nguvu na wanapata faida nyingi sana.

Kuna nafasi kubwa ya ajira katika soka, dada zetu wakifanikiwa kucheza Kombe la Dunia, itakuwa ni rekodi, itakuwa ni nafasi nzuri ya kulitangaza taifa na mpira wa wanawake wa Tanzania na faida hizi, zitaendelea kudumu katika vizazi vyetu kwa kuwa watakuwa wamefungua njia ya timu za Ulaya, Amerika na Asia kuja kusajili wachezaji mbalimbali ambao watakuwa wamefungua pia njia ya ajira.


Ushindi dhidi ya Burundi ni jukumu la Watanzania wazalendo na raha unaona TFF wameweka viingilio vya chini kabisa. Unaona kwa VIP A ni Sh 5,000, VIP B ni Sh 1,000 na bure kwa watu wote watakaoingia mzunguko, wao wataingia bure kabisa.

Vipi ishindikane kwenda kuwaunga mkono ndugu zetu, wadogo zetu na unaona wanalipigania taifa na tumeona mechi nyingi namna ambavyo wamekuwa wakipambana na kutupa sifa mara kadhaa? Huu ni wakati mwingine wa kuwaunga mkono na kuwaonyesha kweli tumekuwa nao na tuko nao kwa ajili ya taifa letu. Haya twende zetu taifa, tukawaunge mkono dada zetu. 
SOMA NA HII  KINACHOWAKOSESHA NGUVU KIPINDI CHA PILI WACHEZAJI WA NAMUNGO HIKI HAPA, DAWA YA AZAM YAANDALIWA