Home Uncategorized KAPTULA YA ZAHERA HAIWEZI KUWA ISHU, TWENDENI NA MAMBO YA MSINGI

KAPTULA YA ZAHERA HAIWEZI KUWA ISHU, TWENDENI NA MAMBO YA MSINGI

NA SALEH ALLY
KILA mmoja anaweza kuamua kusikiliza hadithi anayoamini inaweza kumfurahisha lakini wakati mwingine unalazimika kusikiliza ile usiyoipenda ili kujua jambo.

Hadithi inayovutia masikio ni ile inayofurahisha ubongo na kutengeneza matamanio ya moyo na mwisho ni furaha. Hadithi inayoudhi, mwisho inatengeneza maudhi lakini ukiichukulia chanya, unatengeneza jambo linaloweza kuwa jema mbele.

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), wameamua kuunda na kuboresha kanuni zao kuhusiana na suala la kutaka makocha wawe na nidhamu na wametoa kila kitu wazi kwamba wawe na mwonekano nadhifu.

Unadhifu huu, unaonekana kuzua mjadala mkubwa hasa kwa kuwa mmoja wa makocha wa timu kubwa Tanzania, ameadhibiwa.

Mwinyi Zahera amekumbana na adhabu ya Sh 500,000 pamoja na kufungiwa mechi tatu. Hili jambo limeonekana kuwakera wapenda mpira wengi hasa mashabiki wa Yanga.

Nakumbuka siku chache zimepita nikiwa katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam, vijana waendesha bajaji walinisogelea na kulalamika kwamba walikuwa wanaonewa na wanaamini Yanga inahujumiwa.

Jiulize hujuma ni ipi hasa? Mfano angekuwa ameadhibiwa kocha wa Ruvu Shooting, ingekuwa ni hujuma? Lazima jibu ni hapana.


Zahera mwenyewe amekiri kwamba alikuwa analijua hili suala kwa kuwa aliambiwa na meneja wa timu dakika chache kabla ya kwenda uwanjani. Lakini yeye akawa ameshachelewa kubadili nguo na muda haukuwa unamruhusu.

Hapa utaona, kosa ni la ndani ya Yanga, waliochelewa kumueleza kocha kuhusiana na hilo. Lakini pia utajiuliza vipi hakujua kabla hadi siku ya mechi? Bado suala la uzembe linabaki ndani ya klabu.

Kama kanuni imepitishwa, na inaeleweka kuna haja gani ya kuingiza malumbano badala ya kuitekeleza? Kwani nani anabisha kwamba hata England makocha wanatakiwa kuwa nadhifu?

Inajulikana nguo za kimichezo, zile bukta ambazo benchi la ufundi lilivaa sare inayofanana inatambulika. Kama kocha anataka kuvaa tofauti na benchi la ufundi, basi avae nadhifu.

Zahera anaweza kuwa anavutiwa na kaptula ya Polo lakini sahihi avae suruali nadhifu na jambo hili amekuwa analifanya mara kadha wa kadha huko nyuma.

Kitu kizuri zaidi, Zahera mwenyewe hakukataa hata kidogo kuhusiana na kuvaa kama alivyotakiwa na akasisitiza anazo suti kadhaa ambazo anaweza kuvaa.

Ninaamini Zahera anazo nguo na sote tunaelewa nguo za aina gani, hivyo hakuna sababu ya msingi inayotulazimisha kuutanua mjadala na kutaka kuzungumza masuala yasiyokuwa na sababu za msingi.

Ndiyo maana nimesisitiza hili ni jambo dogo sana ambalo kiuhalisia tunapaswa kukubaliana nalo, Zahera mwenyewe amekubaliana nalo halafu tuendelee mbele. Na huenda ndani ya mjadala huu, jambo la msingi nililiona kuwa ni adhabu kuwa na “hasira” bila sababu za msingi.


Hasira hizo katika mjadala huu na ambacho ninaamini TPLB nao wanaweza kuliangalia tena ni adhabu za mechi tatu kutokana na kuzungumza ambacho wanaona si sahihi, ni kubwa sana kwa kocha ambaye anafundisha timu ya ligi kuu.
Najua faini ya Sh 500,000 ni kutokana na suala la mavazi. Ambayo pia naona ingeweza kuwa katika mwendo usiolazimisha kukomoa au kuumiza.

Hakukupaswa kuwa na adhabu za kukomoa na adhabu inatakiwa kuwa na “matundu ya pua”. Yaani iwe kupumua na kurekebisha mambo kulingana na hali.
Mfano iseme, faini Sh 300,000 na onyo kali na akirudia, adhabu ni Sh 500,000 faini pamoja na mechi tatu. Hii ni kuonyesha adhabu hailengi kumkomoa mtu badala yake kufanya vitu sahihi na bora.

Atakayerudia baada ya hapo hata adhabu ikipanda, basi inakuwa sahihi kabisa. Hili ndilo jambo linalopaswa kuwa muongozo wa adhabu inayoweza kujenga au kuwakumbusha watu kwa nia njema.

Adhabu ya kufungiwa mechi tatu kwa kuanzia kwa ajili ya kuzungumza pia ni kali sana kwa kuwa pia mpira hautaki ukali uliopitiliza isipokuwa kwa watukutu. Asili ya adhabu huendana na onyo au katazo na baada ya hapo inafuatia.


Bodi ya ligi haiwezi kuwa ile inayoadhibu kila kukicha. Tunapaswa kujifunza na kurekebisha mambo ili kwenda katika mabadiliko au mafanikio.











SOMA NA HII  KIFAA MAALUMU CHA MORRISON MAZOEZINI CHAIBUA GUMZO