Home Uncategorized KAGERA SUGAR: MASHABIKI NJOONI MUONE BURUDANI MBELE YA YANGA

KAGERA SUGAR: MASHABIKI NJOONI MUONE BURUDANI MBELE YA YANGA


MECKY Maxime, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar hajawa na matokeo mazuri kwenye mechi zake za Ligi Kuu Bara ndani ya mwaka mpya 2020 kwa kuwa hakuna mechi hata moja aliyoambulia pointi tatu tofauti na alivyoanza ligi  kwa kasi.

Kagera Sugar ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Biashara United Agosti 24,2019, kisha ilishinda mbele ya Allliace kwa mabao 2-1 Septemba 15 na Septemba 21 ilishinda bao 1-0 mbele ya Mbao FC kisha ilipokea kichapo mbele ya Simba mabao 3-0, ikachapwa mbele ya JKT Tanzania bao 1-0 ikarudi kwenye ubora na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Tanzania Prisons.

 Mbeya City iliyokuwa chini ya Juma Mwambusi ilichapwa mabao 4-1 Oktoba 24, ikaichapa Namungo mabao 2-0 Oktoba 30, ikalazimisha sare ya bila kufungana na Azam FC Novemba 11 ikaichapa KMC mabao 2-1 Novemba 11 na ikaichapa Lipuli mabao 2-1 Novemba 22.

Kichapo cha mabao 3-1 mbele ya Mtibwa Sugar Novemba 26 kiliwapunguzia tena kasi wakaibukia na sare ya bila kufungana na Ndanda Novemba 29 na mchezo wao wa kufungia mwaka 2019, Desemba 30 walichapwa mabao 2-1 na Ruvu Shooting. Vijana wa Maxime walifungua mwaka 2020 kwa kichapo cha bao 1-0 mbele ya Coastal Union ilikuwa Januari,8 2020 na wakachapwa mabao 2-1 na Polisi Tanzania Januari 11 na kuifanya Kagera Sugar kupoteza mechi zake zote tatu ilizocheza ikiwa ugenini kwa kichapo.

Leo ana kibarua dhidi ya Yanga ambayo imetoka kulazimisha sare ya mabao 2-2 na Simba kwenye mchezo wa ligi, Championi Jumatano limefanya mahojiano na kocha Maxime ili kuja wapi ana kwama na mipango yake kwa sasa ipo wapi, huyu hapa:-
“Kagera Sugar tupo vizuri tunajua kupambana na kila aina ya timu na matokeo yote machungu na mazuri tunayaambua hatuna mashaka katika hili na tunajiamini.
Haujapata pointi tatu kwenye mechi zako za karibuni kwa nini?
“Nimefungwa na wapinzani wenzangu kama ambavyo nami nilikuwa ninawafunga. Huu ni mpira na ndani ya dakika tisini tunapata matokeo ya kile tulichokifanya.
“Haimaanishi kwamba sikustahili ushindi hapana ni mbinu na aina ya mchezo ambayo ninakutana nayo. Licha ya kufungwa vijana wanacheza mpira hapo kuna kitu ambacho ninajifunza na ninajivunia.
Unadhani tatizo lipo wapi ndani ya timu?
“Hakuna tatizo lolote ndani ya timu kwa sasa. Natazama ushindani ulivyo na ninatazam vitu ambavyo wanavifanya uwanjani ninapenda na nina amini watarejea kwenye ubora wao.
Una mgogoro wowote na wachezaji wako?
“Hilo halipo nina amani kabisa na ninafanya nao kazi kwa ukaribu kuona namna gani tunapata matokeo kwenye mechi zetu ambazo tunacheza.
Mchezo wako na Yanga unautazamaje?
“Ni mchezo mzuri na utakuwa mgumu pamoja na ushindani kwani wapinzani wetu wapo vizuri nasi pia tupo vizuri hivyo naona kuna kitu kizuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga.
Unadhani kushindwa kwako kupata matokeo kwenye mechi za karibuni kutakupa ugumu kupata matokeo?
“Mechi za nyuma zimeshapita tunaachana nazo tunatazama ile iliyopo mkononi hiyo ndiyo muhimu nayo ni dhidi yetu na Yanga. Hapo hakuna tunachohitaji ni ushindi kwani Yanga ni timu sawa na zilivyo timu nyingine tofauti yao ni ukongwe na uzoefu wa wachezaji walionao.
Ushindani wa ligi upoje?
“Mkubwa na ninaupenda kuuona ukiendelea na kwa sasa nasi pia tupo kwenye huo ushindani.
Mashabiki unawaambiaje?
“Mechi yetu dhidi ya Yanga itakuwa ngumu ila nawaambia kwamba waje uwanjani wapate burudani wataona namna mpira unavyochezwa na watafurahi. Waambie wasikose kuja kuona burudani,” anamaliza Maxime.
SOMA NA HII  KMC WATAJA SABABU YA KUPOTEZA MBELE YA AS KIGALI LEO TAIFA