Home Uncategorized KUNA JAMBO LA MUHIMU KWA YANGA KWA SASA WANATAKIWA KULIFANYA MBELE YA...

KUNA JAMBO LA MUHIMU KWA YANGA KWA SASA WANATAKIWA KULIFANYA MBELE YA GSM, WAKICHEMKA BASI YA MANJI YATAENDELEA KUISHI


KUNA matawi mengi maarufu ya Klabu ya Simba, lakini lipo taji moja lina umaarufu mkubwa na maana kubwa sana kwa mpira wa kisasa. Tawi hilo linaitwa Mpira Pesa.
Hili ni tawi ambalo hata mashabiki wa Yanga wanatakiwa kulipenda. Ndio, wanatakiwa kulipenda Tawi la Mpira Pesa. Ni tawi lenye maana kubwa sana kwenye mpira wa kisasa.
Pamoja na vitu vingine muhimu sana, lakini mpira unahitaji pesa kwanza. Yanga imepitia kwenye mikono mingi sana ya watu wenye pesa lakini waliondoka na kuiacha Yanga masikini.
Yanga haijawahi kuwa tajiri lakini imewahi kuongozwa au kusaidiwa na watu wengi sana wenye pesa.
Wakati Yanga wanafanya uchaguzi wao huu waliompa Dkt Mshindo Msolla nafasi ya uenyekiti, nilidhani amekuja kwa jambo moja tu. Nilidhani amekuja kama msomi kuwapa zawadi wana Yanga.
Yanga kwa zaidi ya miaka 80 imemkosa mtu wa kuwapa zawadi. Imemkosa mtu wa kuijengea misingi klabu hii kujitegemea kiuchumi! Hili tu ndiyo jambo kubwa ambalo Yanga imelikosa kwa miaka yote zaidi 80.
Yanga haijawahi kushindwa kushinda mataji ya ndani. Yanga haijawahi kukosa mashabiki kila inakokwenda. Lakini Yanga haijawahi kujitegemea kiuchumi. Ni timu kubwa inayoishi kwa zaidi ya miaka 80 kwa kutegemea mifuko ya watu mbalimbali.
Mpira Pesa ni Tawi la Simba ambalo linaweza kuibadilisha Yanga. Hili tawi lina jina linalosadifu kitu wanachohitaji Yanga. Kumekuwa na swali gumu sana la mtu au kampuni inayoweza kuja kuwekeza Yanga baada ya Yusuph Manji kuiacha Yanga.
Watu wanajiuliza, hata kama Yanga itakwenda kwenye mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ni tajiri gani yuko tayari kuwekeza Yanga? Hili ni swali ambalo watu kama GSM waanze kutoa majibu.
Mpira Pesa ndiyo unapaswa kuwa wimbo kwa wana Yanga kwa sasa. Kwa mfumo huu walionao kwa sasa haujawahi kuiacha Yanga tajiri.
Hawa GSM wanakuja kama alivyokuja Abbas Gulamali, wanakuja kama alivyokuja Manji! Njia ni zile zile lakini mwenyekiti asipochangamka na kuwatengenezea mfumo wa uwekezaji wa kisasa na wao wataondoka.
Hata leo hii GSM wakijitoa Yanga, timu inarudi kulekule! Kazi ya Mwenyekiti wa Yanga kwa sasa ilipaswa kuwa rahisi tu. Anapaswa kuitisha kikao na kamati yake ya utendaji na kisha mkutano mkuu wenye lengo la kuwaomba wanachama wakubali klabu iende kwenye mabadiliko.
Wanachama lazima wapewe elimu ya kutosha juu ya mabadiliko hayo na waridhie. Bila shaka yoyote sioni kama wanachama watakataa jambo hili. Angalau kila mwana Yanga anaona mabadiliko waliyonayo Simba kwa sasa.
Yanga wakiwa makini, wanaweza hata kufanikiwa zaidi na kwa haraka kuliko hata Simba. Mpira wa maneno umekwisha, hauwezi kuongoza timu bila pesa.
Kampuni ya GSM ndiyo inayofanya karibu kila kitu kwa Yanga hii. Kuanzia usajili wa wachezaji na makocha mpaka mishahara. Ni njia zilezile za kina Abbas Gulamali. Ni njia zilezile za kina Yusuph Manji. Ni watu wa muhimu sana kuwashikilia.
Mwenyekiti wa Yanga asisubiri mpaka na wao wamechoka kumwaga pesa ndiyo akaibuka na hoja ya mabadiliko. Muda unaokubalika ni sasa. Hakuna mtu aliyefanikiwa kuiongoza timu ya mpira zama hizi bila kuwa na pesa.
Yanga watakuwa wanajidanganya kama watakataa mabadiliko. Ni uongo wa levo ya PHD kuamini kwamba wawekezaji wa wananchi ni wananchi wenyewe.
Hii ni moja ya kauli mbiu ya uongo kabisa. Yanga imekuwepo miaka zaidi ya 80 kwa wananchi na hakuna chochote cha kiuchumi kilichowahi kuibeba timu.
Kampuni ya GSM sio wajinga, wanajambo lao. Hakuna mtu kwenye zama hizi ambaye yuko tayari kumwaga pesa tu.
Kila mtu anaijua pesa. Kila mtu anaipenda pesa. GSM ni wafanyabiashara, kama wana Yanga wanadhani jamaa wanafaa, wapeni makubaliano ya kibiashara ya uendeshaji wa klabu yenu.
GSM watakapoona kwamba hakuna chochote, nao watatoweka. Mwenyekiti wa Yanga huu ndiyo muda wake wa kumwaga karata dume kwa wanachama. Ndiyo muda wa kuitisha mkutano mkuu wa wanachama kabla GSM nao hawajakimbia.
Habari za kuendelea kudanganyana kwamba muwekezaji wa wananchi ni wananchi wenyewe ni uongo wa daraja la juu sana ambao haujawahi kuisaidia Yanga.
Zama zimebadilika na Yanga wanatakiwa kubadilika. Narudia, hawa GSM sio wajinga ndiyo maana ni matajiri. Wanajua kufanya biashara, kama Yanga haiwalipi wanaweza kuondoka.
Ndiyo tabia za wafanyabiashara. Hawa ni watu wa kuwashika mkono. Sio lazima hata wapewe timu peke yao, mnaweza kupata wawekezaji zaidi ya mmoja na wao wakiwemo.
Kazi ya mwenyekiti wa klabu kama hana pesa ni lawama tupu. GSM kwa sasa nadhani wanafanya mambo makubwa kuliko hata kamati ya utendaji ya klabu.
Kwa mpira wa kisasa, unaweza kuwa shabiki wa Yanga, lakini ukalipenda Tawi la Simba la Mpira Pesa!
SOMA NA HII  AJIBU AFUNGUKA NAMNA REKODI ZA YANGA ZINAVYOMTESA