Home Uncategorized NIDA YAZUA BALAA SHINYANGA, KIGOGO ATIWA MBARONI

NIDA YAZUA BALAA SHINYANGA, KIGOGO ATIWA MBARONI


OFISA  Msajili Msaidizi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida),  mkoani Shinyanga, Haruna Mushi,  na wakala wa usajili laini za simu za mkononi, Victor Isack Vincent, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwatoza fedha wananchi kiasi cha Shilingi 30,000 kila mmoja ili wawapatie namba za Nida na kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole.

Tukio hilo limetokea jana Jumatatu Januari 20,2020,  majira ya saa saba mchana wakati mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alipofika kwenye ofisi za Nida mjini Shinyanga baada ya kupata taarifa za wananchi kuombwa fedha ili wapate namba hizo.

Akielezea tukio hilo, Mboneko, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Shinyanga, alisema wakati akiwa kwenye ofisi hizo za Nida, alipata taarifa za wananchi kuombwa pesa kutoka kwa  ofisa huyo.

Alisema mara baada ya kumkamata wakala huyo  na kuanza kumhoji kwa nini alikuwa anatoza fedha wananchi ili awapatie namba  wakati yeye si mtumishi wa Nida,  akasema huwa anashirikiana na mmoja wa maofisa na Nida.

“Baada ya kumkamata akamtaja  Haruna Mushi kuwa wanashirikiana naye kuomba fedha wananchi, ambapo yeye ndiyo mtoaji wa namba za Nida, na wakala huyu wa simu ndiyo mkusanyaji wa fedha.”

“Tulipopewa taarifa hiyo ikabidi tumkamate  Haruna Mushi, ambapo tumefanya uchunguzi wa simu zao na kubaini kuwepo na mawasiliano ya wananchi kuwaomba fedha na baadhi yao wameshatuma fedha hizo kwenye simu zao, ambapo bado tunaendelea na uchunguzi zaidi,”aliongeza.

Pia Mboneko alitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuacha tabia ya kutoa fedha ili kupata namba hizo kwani serikali inatoa namba hizo bure, ambapo aliwaagiza maofisa wa Nida wafanye kazi usiku kucha na kutofunga ofisi hizo, hadi pale watakapomaliza watu wote kuwapatia namba hizo za Nida.

Naye ofisa usajili  Victor Isaack Vincent, alikiri  kuomba fedha wananchi ili awasaidie kupata namba za Nida kwa kushirikiana na Haruna Mushi, na akaomba msamaha kwa kufanya makosa hayo.

Hata hivyo, Mushi alikanusha tuhuma za kushirikiana na wakala huyo  kuomba fedha wananchi huku akikiri huwa alikuwa anampatia majina ya watu kwa SMS na kisha kumuangalizia namba za Nida.

Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Joseph Paulo, alisema  upelelezi bado unaendelea ambapo wamewakabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ukikamilika watafikishwa mahakamani.
SOMA NA HII  SIMBA YAFUNGUKIA ISHU YA MKUDE KUFUKUZWA SIMBA