Home Uncategorized CORONA YAZIDI KUWA TISHIO KWA WAAFUNZI WATANZANIA, SERIKALI NCHINI YATOA TAMKO

CORONA YAZIDI KUWA TISHIO KWA WAAFUNZI WATANZANIA, SERIKALI NCHINI YATOA TAMKO


Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema wanafunzi wanaosoma katika mji wa Wuhan hawawezi kurudi kwa sababu kuna katazo la kutoingia wala kutoka kwenye mji huo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Hatua hiyo inafuatia baada ya wanafunzi wanaosoma katika mji huo kuiomba Serikali iwasaidie warudi nchini kutokana na kasi ya ongezeko la vifo na maambukizi ya virusi hivyo.

Juzi pekee watu 103 walifariki dunia kutokana na virusi hivyo na kufanya waliofariki dunia hadi sasa kufikia 1,016 lakini maambukizi mapya yameshuka kwa asilimia 20 kutoka watu 3,062 hadi 2,478.

Balozi Kairuki akizungumzia suala la wanafunzi hao, alisema katazo la watu kutembea limesababisha msongo wa mawazo kwa watu wengi wakiwamo wanafunzi hao na kusisitiza lazima wafuate masharti kwa usalama.

“Nimeiona video ya vijana wetu wakitaka waondolewe, ugonjwa upo katika nchi nzima ya China, lakini umeenea zaidi jimbo la Hubei, hasa mji wa Wuhan ambako wako vijana hao.

“Ukifungiwa muda mrefu lazima utakuwa na ‘stress, depression’ na hali hii ndiyo inayopelekea vijana wetu wakitaka waondolewe.

“’Weekend’ nilikuwa na kikao na viongozi wao kwa sababu siruhusiwi kwenda huko na hata hapa Beijing siruhusiwi hata kusogea nje ya geti,” alisema Balozi Kairuki.

Alisema hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia au kutoka nje ya jimbo au mji huo na kila aliyeko ndani anatakiwa kuchukua tahadhari kwa kukaa ndani ya nyumba, kuepuka misongamano na kuzingatia kanuni za usafi.

“Pale inapobidi utoke nje uvae ‘mask’, hakuna treni, basi, ndege wala gari la mtu binafsi linaloruhusiwa kufika kule,” alisema Balozi Kairuki.

Alitoa mfano wa Japan ambayo iliamua kuondoa wanafunzi wake katika mji wa Wuhan, lakini hilo lilisababisha wengine kukumbwa na maambukizi ya virusi hivyo na hadi sasa zaidi ya watu 20 wameathiriwa.

“Hatutaki kurudia makosa yaliyofanywa na Japan matokeo yake tukapeleka ugonjwa nchini kwetu. Japan ilikuwa na wanafunzi Wuhan na wote walikuwa wazima, lakini zoezi lilipoendeshwa baadhi ya wanafunzi walipata virusi vya corona, wakaambukiza wengine.

“Walipofika uwanja wa ndege kuna wafanyakazi walipata ugonjwa, matokeo yake idadi ya wagonjwa imeongezeka na sasa watu zaidi ya 20 wako kwenye karantini.

“Lazima tuwe makini kuhakikisha ugonjwa huu hauji kwenye bara letu, tunawalinda watu wengi zaidi walioko huko.

“Tathmini ikionyesha tunaweza kufanya zoezi hilo kwa usalama, naamini Serikali yetu ni sikivu itachukua hatua,” alisema Balozi Kairuki.

WANAFUNZI

Katika video iliyosambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Watanzania wanaosoma Wuhan walionekana wakiwa na mabango yaliyosomeka ‘Please, please, please’, ‘Dear Tanzania please bring us home, ‘We are not infected yet’.

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaosoma Wuhan, Jacob Julius, alisema wanafunzi hao wanasoma Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ambacho kina Watanzania zaidi ya 200.

“Tunamshukuru Mungu mpaka sasa tuko salama, hakuna ambaye ameugua au amesadikiwa (suspected) kuwa na virusi vya corona.

“Wote tuna shauku ya kutaka kurejea ama kutoka katika maeneo haya na kwenda maeneo mengine ambayo yako salama zaidi, kwa sababu mazingira haya yanaogofya kutokana na vifo na maambukizi kuendelea kuwa makubwa siku hadi siku.

“Lakini hakuna namna nyingine bora ya kufanya zaidi ya kuacha taratibu stahiki kufanyika, mimi ninaamini Mungu ataendelea kutulinda maana kama katulinda hadi sasa basi ataendelea kutulinda,” alisema Julius.

SIMU ZA MOJA KWA MOJA

Ili kuhakikisha usalama na afya ya raia wa kigeni walioko Jimbo la Hubei, Serikali ya China imeanzisha simu za moja kwa moja.

Taarifa ya Ubalozi wa China nchini ilieleza kuwa wameongeza juhudi za kutoa taarifa kwa raia wa kigeni huku wakisisitiza njia salama ni kuendelea kujikinga.

Ubalozi huo pia umekanusha taarifa juu ya kuwapo kwa uvumi ambao umekuwa ukienea nchini kuhusu homa ya mapafu na kuwataka Watanzania kuzipuuza.

“Kuna uvumi kadhaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Tanzania kuhusiana na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.

“Tunawashauri Watanzania kupuuza uvumi huo badala yake waamini taarifa zinazotolewa na mamlaka rasmi kama Wizara ya Afya na Ubalozi wa China nchini Tanzania,” ilieleza tararifa hiyo.

Hadi kufikia Februari 9, mwaka huu watu 40,171 walithibitishwa kuugua na kati ya hao 3,281 walipona na kuruhusiwa hospitalini, 908 walifariki na 35,982 bado walikuwa wakiendelea na matibabu.

CHANZO: MTANZANIA
SOMA NA HII  LUC ATISHIA KUONDOKA YANGA!! CHAMPIONI KATIKA UKURASA WA MBELE LEO JUMATATU