Home Uncategorized KISA YANGA MZAMIRU HALI TETE SIMBA

KISA YANGA MZAMIRU HALI TETE SIMBA


KIUNGO wa Simba, Mzamiru Yassin, ataendelea kuzikosa mechi za timu hiyo, kutokana na kusumbuliwa na tatizo la goti analodaiwa kuumia katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga Januari 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tangu siku hiyo, Mzamiru hajaonekana uwanjani akiwa amevaa jezi nyekundu na nyeupe katika mbio za timu hiyo za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Simba ambao walikuwa hawajui kama Mzamiru ni majeruhi, tayari walikuwa wameanza kuutolea shutuma uongozi wa timu hiyo, wakiutuhumu kuwa umemsimamisha kutokana na kosa la kimchezo alilofanya uwanjani katika mechi dhidi ya Yanga.

Kosa hilo ni lile lililoiwezesha Yanga kupata bao baada ya kupokonywa mpira na Mapinduzi Balama ambaye aliifungia timu yake moja kati ya mabao iliyoyapata kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, Mzamiru ni majeruhi na anaendelea na matibabu ya goti na wala hakuna tatizo lingine dhidi yake.

“Mzamiru ni majeruhi na yupo nje ya uwanja akiendelea kupata matibabu, yeye pamoja na wachezaji wengine ambao ni Miraji Athumani ‘Sheva’ pamoja na Deo Kanda.

“Hata hivyo, hali zao kwa pamoja wanaendelea vizuri na muda wowote pindi watapokuwa wamepona, watarejea uwanjani kuendelea kuitumikia timu yetu, hayo mengine yanayosemwa ni uzushi tu na siyo kweli,” alisema Rweyemamu.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa anawamisi wachezaji hao katika kikosi chake kutokana na majareha yanayowasumbua.

Lakini alisema kuwa, anawaombea waweze kupona haraka na kurudi uwanjani kuendelea kuitumikia timu hiyo katika harakati zake za kutetea ubingwa wake.
SOMA NA HII  HIVI NDIVYO SIMBA ILIVYOIPIGA BAO AL AHLY