Home Uncategorized MAREKANI YASEMA VIRUSI VYA CORONA NI FURSA KWAO

MAREKANI YASEMA VIRUSI VYA CORONA NI FURSA KWAO

KATIBU wa masuala ya kibiashara nchini Marekani, Wilbur Ross, amesema  mlipuko mbaya wa virusi vya Corona nchini China unaweza kuinua uchumi wa Marekani na kurudisha ajira kaskazinimwa mwa nchi hiyo.

Ross ameyasema hayo wakati akihojiwa na kituo cha runinga cha Fox nchini humo kuhusu tukio hilo  ambalo kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo kumezua hofu kuhusu athari zake katika uchumi wa China na ukuaji wake  kwa jumla.

Matamshi hayo yamepokewa kwa hisia kali kutoka kwa wakosoaji wa utawala wa Rais wa Marekani, DonaldTrump. Akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa kituo hicho kuhusu iwapo mlipuko huo ni hatari kwa uchumi wa Marekani,  Ross alisema:

”Sitaki kuzungumzia kuhusu mafanikio kuhusu ugonjwa huu hatari. Ukweli ni kwamba unatoa fursa kwa biashara. Hivyo basi nadhani utasaidia kuongeza ajira kaskazini mwa Marekani’.”

Baadaye wizara ya biashara nchini humo kupitia msemaji wake, iliunga mkono matamshi yake  kwamba: ”Kama waziri Ross alivyoweka wazi,  kitu cha kwanza ni kuhakikisha kuwa virusi hivyo vinadhibitiwa na baadaye kuwasaidia waathiriwa wa ugonjwa huo. Pia ni vyema kutazama athari za kufanya biashara na taifa ambalo lina historia ya kuzuia hatari nyingi kwa watu wake na dunia nzima kwa jumla.” 

Matamshi hayo yamekosolewa sana huku mbunge wa chama cha Democrat, Don Beyer, akiandika katika akaunti yake ya Twitter na kuuliza ni vipi mtu anaweza kuchukua fursa ya kibiashara katika mlipuko wa janga kubwa!

Wanauchumi pia wameuliza maswali mengi kuhusu matamshi ya  Ross.

Simon Baptist kutoka kitengo cha ujasusi cha Singapore aliiambia BBC kwamba matamshi hayo yalimshangaza.

“Kampuni hazitaweza kupata uwekezaji wa kipindi kirefu kutokana na mlipuko ambao huenda ukaathiri watu kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita,” alisema.

Aliongeza kwamba virusi hivyo huenda vikawa na athari mbaya badala ya nzuri:  ”Ukweli ni kwamba Marekani itapoteza sana kwa sababu licha ya kila kitu China ni soko lake kubwa, hivyo basi iwapo uchumi wa China utapunguza kasi katika ukuaji wake utaathiri pakubwa uchumi wa Marekani vilevile.”

Virusi hivyo vipya vimetajwa kuwa janga la kiafya na shirika la afya duniani (WHO) huku vikiendelea kusambaa nje ya China. Takriban watu 213 wamefariki kutokana na virusi hivyo nchini China na sasa vimesambaa hadi katika mataifa 18 mengine duniani.

Wanauchumi wamesema kwamba virusi hivyo vya Corona vinaweza kuwa na athari kubwa katika uchumi kuliko virusi vya SARS vilivyozuka kati ya 2002-2003. SARS iliambukiza watu 8,000 na kusababisha vifo vya watu 700 na inakadiriwa kuugharimu uchumi duniani kwa takriban Dola bilioni 30.

Virusi vya Corona vimelazimu kampuni mbalimbali duniani zikiwemo zile za teknolojia, watengenezaji na wauzaji wa magari kufunga shughuli kwa muda nchini China huku mamlaka ikiendeleza likizo ya kusherehekea mwaka mpya na kuweka vikwazo vya usafiri katika taifa hilo.
SOMA NA HII  SIMBA YATAJA SABABU YA KUSHINDA LEO MBELE YA NDANDA FC