Home Uncategorized WALE WENYE TABIA ZA WAWA NA MORRISON TUWAKEMEE KWENYE LIGI ZOTE, HATUA...

WALE WENYE TABIA ZA WAWA NA MORRISON TUWAKEMEE KWENYE LIGI ZOTE, HATUA ZICHUKULIWE

JANUARI 4,2020 mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa kwa wapinzani wa jadi Yanga na Simba mzunguko wa kwanza uliacha matukio mengi tata ambayo yaligeuka gumzo kwa kila mwanamichezo.
Mchezo huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa ulitawaliwa na tambo za kutosha kwa kila timu kuamini itaibuka na ushindi mwisho wa siku baada ya dakika 90 ikawa ni 2-2.
Ukiachana na matokeo ambayo yalitokea uwanjani na kelele kutawala kuna matukio ambayo yaliacha maswali na mpaka sasa bado hayajajibiwa ikiwa tayari muda wa siku 47 zimeshameguka.
Kuna ishu ya beki kisiki ndani ya Simba raia wa Ivory Coast, Pascal Wawa kumchezea rafu mshambuliaji wa Yanga, Ditram Nchimbi wakati wa harakati za kuokoa hatari.
Uzuri ni kwamba tukio hilo lilinaswa na Azam TV ilionesha kwamba Wawa alikuwa akimkanyanga Nchimbi aliyekuwa ameanguka chini na hakuna hatua ambayo imechukuliwa.
Kamati ya masaa 72 ilichukua hatua na kutoa onyo kwa waamuzi wa mchezo huo huku suala la Wawa likiwa kiporo bila kufanyiwa maamuzi.
Kabla halijapoa hilo tena limeibuka lingine la mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison naye alimpiga kiwiko mchezaji wa Tanzania Prisons.
Morrison alifanya hivyo kwa mchezaji wa timu pinzani Februari 16 Uwanja wa Taifa kwa kumpiga kiwiko Jeremiah Juma hili ni balaa jingine.
Mchezo huo wa ligi matokeo yake yalikamilka kwa sare tasa ya bila kufungana.
Kwa kawaida  mlinzi wa mchezaji ndani ya uwanja ni mchezaji mwenzake sasa kama mchezaji ambaye amechezea timu kubwa ikiwa na anatoka nje ya nchi pia anafanya mambo haya wakati kukiwa hakuna purukushani zozote hii ni mbaya.
Tabia hii inapaswa kukemewa na kupingwa kwa nguvu zote na wapenda michezo ili kuongeza usalama wa wachezaji wetu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati zao ambazo huwa zinatoa maamuzi zinapaswa ziyatazame haya matukio kwa ukaribu na kutoa adhabu ambazo zitakuwa fundisho kwa wachezaji wengine.
Huenda kuna ugumu katika kutafuta ushahidi lakini matukio yote yanaonekana dhahiri shahiri na Azam TV wamekuwa makini katika matukio mengi tata ambayo ni ushaidi tosha.
Dunia ya sasa inakwenda kasi sana na kila mmoja anapenda kuvutia kwake rai yangu kwa wachezaji mbinu zao zikifeli kupata matokeo wasitumie hasira kuwaumiza wachezaji wengine.
Tabia hizi zikiwa endelevu zitaondoa ile hadhi ya ubora wa mpira kuwa ni uungwana badala yake itakuwa vita hili sio sawa tabia za wachezaji kama akina Wawa na Morisson zinapaswa zikemewe na zisipewe nafasi.
Kikubwa kwa timu zote zinapokuwa uwanjani zinapaswa zifuate sheria 17 za mpira na waamuzi pia wanapaswa waongeze umakini kwani mpira umekuwa na kasi pamoja na matukio mengi kutokea kwa kasi ya ajabu.
SOMA NA HII  NDAYIRAGIJE WA KMC AMPOTEZA MBELGIJI WA SIMBA