Home Uncategorized LIGI DARAJA LA KWANZA TUSIIFUMBIE MACHO KWANI HUKU MAMBO BADO

LIGI DARAJA LA KWANZA TUSIIFUMBIE MACHO KWANI HUKU MAMBO BADO

MECHI saba kwa sasa ndizo ambazo zimebaki kwa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kumaliza ile ngwe ya kumtafuta mbabe wao atakayepanda Daraja na yule ambaye atashuka.
Kila timu inapambana kwa nafasi yake kutafuta ushindi kwa kuwa hakuna timu inayopenda kubaki pale ambapo ipo kwa muda mrefu ukizingatia kwamba kupanda daraja ni mafanikio.
Ugumu uliopo kwenye kupata matokeo kwa timu zikiwa ugenini unapaswa utafutiwe ufumbuzi wa kudumu kwani imekuwa ni kasumba ambayo inadumu miaka mingi ndani ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kikubwa kwa timu ambazo bado zipo nafasi ya chini kwa sasa ni lazima benchi la ufundi kutafuta mbinu mpya itakayowapa matokeo mazuri ndani ya mechi ambazo watacheza kwa sasa.
Lala salama ya sasa iwe ni ya faida kwa kila timu kupata kile inachostahili bila kuwepo kwa malalamiko ambayo yamekuwa yakiripotiwa na wengi hasa wanaokwenda viwanjani na wakati mwingine wachezaji wenyewe.
Ikiwa kila siku kutakuwa na matokeo ya ugomvi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza ina maana kwamba msingi wa kwanza wa kuwa na timu bora na imara unavunjika
Tukumbuke kwamba kupanda kwenye ligi ni ndoto za timu nyingi shiriki kwenye Ligi Daraja la Kwanza ila mbinu ambazo inaelezwa kuwa zinafanyika sio sawa.
Hali ya sasa ni mbaya kwenye mechi zinazoendelea kuchezeka hivyo umakini unahitajika kwa waamuzi na wasimamizi wa mechi hizi kuona namna gani matokeo yatapatikana kwa usawa.
Kwenye Ligi Kuu Bara kuna ushindani wa kupata ushindi na kinachopiganiwa huku ni kombe na kwa timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza zinahitaji kupanda mpaka kushiriki ligi.
Kitu kizuri ambacho kinahitajika ni kuona kwamba kila timu inapata matokeo ambayo yanastahili bila kuwa na mpango wowote wa kuyapanga na hasa wakati zinapokuwa nyumbani kucheza.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mbali na kuitazama Ligi Kuu Bara kwa ukaribu kuna umuhimu wa kutazama na mwenendo mzima wa Ligi Daraja la Kwanza.
Endapo jicho kubwa litakuwa ndani ya ligi pekee na kuacha huku kwenye kiwanda cha kutengeneza timu shiriki bila kujali maisha yao itakuwa ni hatari kwa afya ya soka letu.
Ili soka liendelee ni lazima kuwe na misingi makini ambayo inaanzia huku chini na haijengwi kwa kubahatisha bali mipango makini na hesabu zenye uhakika.
Timu shiriki ndani ya Ligi Daraja la Kwanza ni lazima zitambue namna gani zinaweza kufikia malengo yao hasa ukizingatia kwamba siku zinakwenda na muda wa ligi kukamilika upo karibu.
Zile ambazo zinaamini kwamba zina nafasi ya kupenya na hazina mtu wa kuzitazama zina jukumu la kutazama mbinu pekee ya ushindi kwenye mechi zao.
Njia ya kupata ushindi kwao ni moja tu kupambana na kufanyia kazi makosa yao ambayo waliyafanya kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi.
Ni safari ndefu ya kuvuka mlima wa Ligi Daraja la Kwanza na kuibukia ndani ya Ligi Kuu Bara ambayo nayo ushindani wake pia ni mkubwa.
Nidhamu kwa wachezaji kwenye mechi zao zote bila kujali wanacheza na nani ni mbinu za kuwafanya wawe makini na bora kwenye matokeo ambayo wanayapata kwenye ligi.
Endapo hakutakuwa na nidhamu kwa wachezaji itasababisha wengi washindwe kufikia malengo kwani mchezo wa mpira ni kitu ambacho kinawategemea wachezaji na mashabiki nao wana mchango wao pia.
Imekuwa ikiripotiwa kuwa kuna baadhi ya mechi ambazo mashabiki wamekuwa wakipata tabu kwa kusukumwa ama wakati mwingine kuumizwa kisa kusapoti aina ya timu ambayo wanaona inafaa.
Kwa hali hii kama ni kweli watu wanaochukua sheria mkononi kisa timu ya mpinzani wake huo sio ushabiki bali ni ujinga ambao unapaswa uachwe mara moja..
Ugomvi haujawahi kuleta furaha kwa mashabi na amani kwa wachezaji kwani ni jambo ambalo hakuna anayependa kuliona hata makocha pia.
Nchi yetu ya Tanzana ni amani na upendo sasa kwa mambo ambayo yanatokea yanaleta picha ambayo sio nzuri ni lazima kubadilika katika jambo hili.
Waamuzi ambao wanasimamia sheria 17 ni muhimu kutazama namna bora ya kuzidi kuwa bora na kuepuka lawama ambazo wamekuwa wakiachiwa na makocha pamoja na wachezaji baada ya mechi kuisha.
Muda sahihi wa kutazama maamuzi ni kujifunza kupitia makosa na kukubali kuyaacha hasa pale ambapo inatokea kwa bahati mbaya.
Makosa yapo kwa kuwa binadamu anafanya makosa ila inapotokea kila mara hili linakuwa sio kosa tena bali ni janga kwa kuwa hakuna ambaye anakuwa anajali.
Njia pekee ya timu kupata ushindi ndani ya dakika tisini ni kupambana ndani ya uwanja ili kupata ushindi kwa uhalali bila kujali aina ya timu ambayo unakutana nayo uwanjani.
Kazi kubwa ya kupambana ipo mikononi mwa wachezaji wenyewe na wanatakiwa kuzifuata mbinu za mwalimu anazowapa muda wa mazoezi ya timu.
SOMA NA HII  MORRISON, MASHINE MPYA YA YANGA YAZUNGUMZIA ISHU YA USHINDANI WA NAMBA