Home Uncategorized MADUDU YA LIGI DARAJA LA KWANZA YASIFUMBIWE MACHO, MFUMO WA PLAYOFF UBORESHWE

MADUDU YA LIGI DARAJA LA KWANZA YASIFUMBIWE MACHO, MFUMO WA PLAYOFF UBORESHWE

LIGI daraja la Kwanza inazidi kumeguka taratibu na ushindani wake unazidi kushika kasi kila iitwapo leo kwa timu shiriki kuonyesha kile wanachokihitaji.

Tunaona kwamba kila timu kwenye kundi lake haikubali kushindwa yaani leo ikifeli kupata matokeo mazuri mchezo unaofuta lazima itapambana na kupata ushindi ama sare.
Hiki ndicho ambacho kinahitajika kwenye maisha ya soka ili kuweka ushindani mzuri na kufanya ligi ichangamke kwa kasi kwenye kila mechi bila kupumzika.
Kwa timu ambazo hazitajipanga vema kwenye hii lala salama matokeo yataonekana uwanjani kwani mchezo wa mpira hauna kificho mambo ni ndani ya uwanja.
Upinzani ulioko Daraja la Kwanza ni mkubwa kuliko ule wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na ukweli kwamba huku timu zinahitaji kupanda kwa udi na uvumba ila  kwenye ligi timu zinapambania ubingwa.
Haina maana kwamba ndani ya ligi kuu hakuna ushindani hapana ninazungumzia hapa namna mbinu zilivyo huku chini na ushindani ulivyo mkubwa.
Mfano mzuri ni kwa timu ambazo ziliwahi kufanya maajabu ndani ya ligi ziliposhuka huku zinapata taabu kurejea mfano mzuri ni Njombe Mji, Pamba SC, Majimaji na Stand United ambazo zote zimekuwa timu za kawaida.
Kumekuwa na mchezo mbaya wa matokeo kwenye mechi nyingi zinazochezwa hasa nyumbani timu nyingi zinashinda kwa matokeo ya ajabu.
Matokeo inaonekana yanapangwa kwa timu za nyumbani ili kuzipa unafuu wa kuendelea kubaki kwenye ushindani na kupata nafasi ya kupanda daraja.
Katika hili sio jambo la kukaa kimya na kusubiri ni kitu gani ambacho kitatokea hapo baadaye zaidi ni kuchukua hatua na kutafuta mianya ilipo kwa sasa ndani ya Ligi Daraja la Kwanza.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatakiwa ilitazame hili kwa ukaribu na kuchukua hatua kwa upesi ili kuondoa zile kelele na maonezi kwa wachezaji na timu.
TFF isifumbie macho huku kwenye Ligi Daraja la Kwanza ni busara pia maamuzi yanayotolewa yakawa ni kwa mujibu wa sheria bila upendeleo.
Kwa upande wa waamuzi inaonekana kwamba bado kuna tatizo la kusimamia sheria 17 za soka ni muhimu kulifanyia kazi hili pia.
Waamuzi wanajua wanachofanya kwa sasa ndani ya Ligi Daraja la Kwanza kutokana na malalamiko kuongezeka kila iitwapo leo kwenye mechi ambazo wanasimamia.
Matokeo inaonekana yanabebwa mfukoni na mwisho wa siku timu inaingia uwanjani ikiwa na uhakika wa kushinda mechi yake kwa namna yoyote ile hasa ikiwa nyumbani.
Hii sio sawa kwani inaua ule ushindani ambao unapaswa uendelee kwenye ligi hii ambayo inatengeneza timu ambayo itashiriki Ligi Kuu Bara na baadaye kuweza kushiriki michuano ya kimataifa iwapo itapata nafasi.
Iwapo itavuka kigingi cha kupanda daraja kwa kutumia mbinu ambazo si salama italeta matokeo mabaya pale watakapokuwa kwenye ligi kuu kutokana na matokeo ambayo watakuwa wanayapata.
Itasababisha matatizo kwao na mashabiki kwani timu ikipanda kwa kutumia mbinu mbaya itavuna matokeo mabaya kwenye mechi zake itakazocheza na itashuka daraja na kuanza kuhangaika kurejea ndani ya ligi kuu tena.
Ugomvi kwenye mechi za sasa unaotokea kwenye mechi ni mbaya kwani inapoteza maana halisi ya mchezo kuwa burudani na badala yake inakuwa uwanja wa fujo.
Chuki ambayo inatengenezwa kwa sasa kwenye hizi mechi ni lazima ikomeshwe ili kurejesha furaha na kurudisha heshima kwenye soka letu ambalo linazidi kukua taratibu.
Zogo sio kitu kizuri kwa wanafamilia ya michezo ni kitu cha msingi kuweka heshima na adabu kwenye kila mechi ambazo zinachezwa bila kujali ni mchezo wa aina gani.
Imani yangu iwapo waamuzi wataamua kusimamia sheria 17 za mpira tutapata timu bora na imara kutoka chini na zikipanda zitaleta ushindani wa kweli.
Maamuzi yawe kwa uhakika eneo la penalti iwe penalti na sio pale ambapo kuna penalti inakuwa faulo na kwenye faulo inakuwa penalti hili ni balaa.
Ligi inaenda ukingoni kwa sasa ni muhimu kuona kila timu inapata kile ambacho imepanda kwani hakuna mchezaji ambaye anapenda kuona timu yake inashindwa kufikia malengo yake.
Kila timu itakayopambana na ipate matokeo kulingana na kile inachokifanya ndani ya uwanja jambo ambalo litafanya hata timu ikipanda iwe katika ubora wake.
Watakaobebwa ni wazi kabisa mambo yatakuwa magumu wakati ule watakaopanda ndani ya ligi na watashindwa kufikia mafanikio yao.
Tunaona pia kuna mechi za Playoff ambazo zinachezwa baada ya ligi kukamilika ila nina ona mfumo unaotumika bado haujawa rafiki.
Timu ambazo zinashiriki kwenye mechi ya kumtafuta mshindi wa Playoff zinakuwa zimetofautiana kwenye madaraja pamoja na muda wa kucheza mechi zao hasa ukizingatia kwamba wengine huwa wanakuwa wamemaliza ligi na kupata muda wa kupumzika.
Hili linapaswa lifanyiwe kazi na TFF kwa kutazama namna mpya ya kumpata mshindi ambaye ataweza kupata ushindi kwa haki bila mazingira ya kutengenezwa kwa kucheza mechi ambazo mshindi anajulikana.
Mabadiliko ni muhimu kwa timu zote kutambua kwamba hakuna ambaye anahitaji kushinda hivyo waamuzi wanapaswa wasisahau kufuata sheria 17 na viongozi waache makocha wafanye kazi.
SOMA NA HII  KOCHA YANGA AWATAKA WACHEZAJI WAKE KUFUNGA MABAO MENGI