BAADA ya mashabiki wa Simba kumpigia kelele kiungo mkabaji wa timu hiyo, Jonas Mkude kuwa ni tatizo katika kikosi chao kutokana na utovu wa nidhamu huku baadhi yao wakitaka afungashiwe virigo, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ameingilia suala hilo ili kuhakikisha linakaa sawa.
Hivi sasa Mkude yupo chini ya uangalizi mkubwa, katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama ili kuhakikisha anakuwa anabadilika na kuwa mmoja wa wachezaji wa kuigwa ndani ya timu hiyo.
Sven amempatia Mkude programu maalumu ya kufanya katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama kutokana na Virusi vya Corona na kila siku atakuwa akiwasiliana naye ili kuona kama ni kweli anatekeleza kwa kiwango kikubwa programu hiyo.
Akizungumza na Gazeti la Championi, Mkude alisema kuwa hivi sasa hataki tena mchezo, ameamua kuhakikisha anazingatia maagizo yote aliyopewa na kocha wake ili kuhakikisha mambo yanakuwa sawa lakini pia anakuwa fiti.
Alisema maneno mengi yamekuwa yakisemwa dhidi yake, kwa hiyo ili kundokana na maneno hayo ni kukaa kimya na kufanya yale yote ambayo kocha wake amemtaka ayafanye katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama na amekuwa akiwasiliana naye kila siku ili kujua maendeleo yake.
“Kwa hiyo, hivi sasa ninajifua vilivyo ili kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa lakini pia kujiweka fiti.
“Mazoezi ninayofanya kwa sasa ni kutokana na programu ambayo kocha alinipatia, hakika siyo programu ya mchezomchezo inahitaji nguvu ya ziada, lakini ninakomaa ili kuhakikisha ninayatendea haki,” alisema Mkude.