NYOTA wa Lipuli, Daruesh Saliboko amesema kuwa iwapo Yanga watakamilisha dili lake kutua makao makuu ya Jangwani watafurahi wenyewe kwani atatatua tatizo la ubutu wa kucheka na nyavu.
Saliboko kabla ya Ligi Kuu Bara kusimamishwa Machi 17 na Serikali kupisha maambukizi zaidi ya Virusi vya Corona alikuwa ametupia mabao nane na katika hayo alipiga hat trick mbele ya Singida United.
Akizungumza na SpotiXtra, Saliboko alisema kuwa kwa sasa anasubiri dili lake la kutua ndani ya Yanga lijibu ndipo atakapowaonyesha uwezo wake wa kucheka na nyavu.
“Nipo vizuri nikiendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona ila nimekuwa nikiskia kwamba Yanga wanahitaji saini yangu iwapo mambo yatakuwa sawa basi wenyewe watapenda kazi yangu itakavyokuwa ndani ya uwanja.
“Bado sijaona mchezaji wa kunipa changamoto kubwa pale kati kwani uwezo ninao na kipaji pia ninacho itakuwa ni mwendo wa kutupia tu kwani wanachokosa Yanga kwa sasa ni utulivu eneo la katikati ambalo mimi ninalimudu,” alisema Saliboko.