Home Uncategorized AZAM FC YAJITOSA KUWANIA KIFAA CHA CONGO KINACHOTAKIWA SIMBA NA YANGA

AZAM FC YAJITOSA KUWANIA KIFAA CHA CONGO KINACHOTAKIWA SIMBA NA YANGA

UKISIKIA kununua ugomvi ndiko huku sasa. Matajiri wa soka nchini, Azam FC wamejitosa katika vita vya vigogo Simba na Yanga kuwania saini ya straika Mkongomani, Mpiana Mozizi anayekipiga FC Lupopo ya DR Congo.

Mozizi alianza kusakwa na Simba kabla ya Yanga nao kujitosa kama tulivyowapasha juzi Jumamosi, lakini Azam nao wamejitosa kutaka kumsainisha mkali huyo mwenye mabao 11.

Ipo hivi. Awali, Mozizi alikuwa akiwindwa na Simba na taarifa ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba mmoja wa mabosi wa juu mwenye sauti yake pale Msimbazi, alimpigia simu mchezaji huyo na kuzungumza naye kuhusu huduma yake.

Lakini, wakati Simba wakiendelea kufanya mchakato huo taratibu kutaka kumsainisha Mozizi, Yanga waliibuka mafichoni na kumtafuta wakala wa mchezaji huyo pamoja na baadhi ya viongozi wa FC Lupopo ili kumaliza kazi kimya kimya.

Mwanaspoti imedokezwa tayari Mozizi tayari amepokea pesa kutoka Yanga (kishika uchumba), na mara baada ya dirisha la usajili kufunguliwa waende moja kwa moja DR Congo ambapo, straika huyo anaishi na kucheza soka huko ili kumaliza dili lake kabisa.

Kukiwa na mvutano huo wa pande zote mbili Simba na Yanga, kumtaka Mozizi Azam nao wameingia vitani kumtaka straika huyo na tayari Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amewasiliana na Katibu wa FC Lupopo kuona uwezekano wa kumchukua straika huyo haraka kabla ya timu hizo kongwe kushtukia dili.

Azam wameamua kuzungumza na FC Lupopo ili kuwapa urahisi wa kumbeba na tayari wametajiwa dau la kumnasa Mozizi huku wakipewa mawasiliano ili kuwasiliana naye moja kwa moja ili kujadiliana maslahi binafsi na kuziacha kwenye mataa Simba na Yanga.

Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema hakuna timu isiyokuwa katika mipango ya usajili na sio kwamba, wapo kimya bali wanafanya mambo yao kimya kimya na watakuja kutangaza mashine zao mpya baada ya mambo kukamilika.

“Kwetu njia sahihi ambayo tunayo ni kufanya mambo kimya kimya kwa maana hiyo kama tunamfuatilia Mozizi au mchezaji mwengine muda ukifika kama atakuwa mali yetu tutamtangaza, lakini wak ati huu tunaendelea na mipango yetu kimya kimya,” alisema Zakaria.

SOMA NA HII  MARIO BALOTELLI APATA DILI LA MAANA PARMA FC

YAFANYA UMAFIA

Katika kuonyesha Azam wanataka ugomvi, wameingilia pia dili lililokuwa likifanywa na Yanga la kutaka kumnasa beki wa wa kushoto wa Polisi Tanzania, Yassin Mustafa ambaye walimkosa katika dirisha dogo na kuishia kumbeba Adeyun Saleh kutoka JKT Tanzania.

Mwanaspoti limepenyezewa kuwa, Azam imesh amalizana na beki huyo aliyejipatia umaarufu katika Ligi Kuu Bara msimu huu kwa kuupiga mwingi.

Kiongozi wa juu wa Azam amelifichulia Mwanaspoti kuwa amesimamia mwenyewe zoezi la kumsainisha mchezaji huyo mkataba wa miaka miwili ambao, msimu ujao utaanza kuitumikia klabu yetu.

“Nimemsainisha mwenyewe Mustapha na hapa tunasubiri muda muafaka kumtangaza kuwa ni mchezaji wetu kwa maana kama kuna timu nyingine ambayo inamtaka itakuwa ngumu kumsainisha kwani, tumeshamalizana naye,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, Mustapha alipotafutwa alisema asingeweza kusema lolote kwa kuwa mwenye jukumu la kuzungumzia ishu hiyo ni viongozi wa Polisi Tanzania kwani, ndio wenye mkataba naye kwa sasa.

“Kama kweli nimesaini Azam itafahamika tu muda ukifika, ila kwa sasa bado nina mkataba Polisi Tanzania ambao, mwisho wa msimu huu ndio utamalizika kwa maana hiyo siwezi kuzungumza lolote kwa sasa kama nitabaki hapa au kuondoka,” alisema beki huyo mwenye rasta.