Home Uncategorized BODI YA LIGI KUKAA KIKAO KIZITO LEO

BODI YA LIGI KUKAA KIKAO KIZITO LEO

MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania TPLB, Almas Kasongo amefunguka kuwa leo watakuwa na kikao kizito na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujadili tarehe rasmi ambayo ligi zitaanza.
Kasongo amesema wamechukua hatua hiyo baada ya hivi karibuni kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa michezo nchini ambao kila mmoja alikuwa na maoni yake juu ya muundo gani utumike ili kuweza kumalizia ngwe ya ligi ambayo imebaki.
Ligi Kuu Bara ilisimama kutokana na janga la Virusi vya Corona ambapo juzi Rais Dk John Magufuli alitangaza kurejea tena kwa shughuli mbalimbali ikiwemo ya michezo kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Kasongo alisema watakuwa na kikao kizito na viongozi wa juu wa TFF na pamoja na wale wa Bodi ya Ligi lengo ni kujadili na kupata mustakabali na ratiba rasmi ya ligi hiyo lini itaanza kupigwa.
“Tutakutana kesho (leo) Jumamosi sisi kama Bodi ya Ligi na wenzetu TFF ili kujadiliana kwa pamoja nini kifanyike katika kumalizia michezo ya ligi ambayo ilibakia, tunafanya hivyo kwa sababu hapa katikati tulipokea maoni mengi ya wadau wa michezo ambao walikuwa na mawazo tofauti, hivyo tutayapitia maoni hayo ili kupata kitu kimoja,” alisema Kasongo
SOMA NA HII  SIMBA WAFUNGUKA JUU YA KUMSAJILI AJIBU WA YANGA