Home Uncategorized HESABU ZA KAGERA SUGAR ZIPO NAMNA HII, CORONA ILITIBUA MAMBO

HESABU ZA KAGERA SUGAR ZIPO NAMNA HII, CORONA ILITIBUA MAMBO

BADO mambo hajawa shwari kwa sasa kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinaendelea kusambaa kwa kasi duniani huku shughuli nyingi zikiwa zimesimamishwa.
Timu zote Bongo kwa kutii tamko zilisitisha kambi za wachezaji ikiwa ni pamoja na Kagera Sugar iliyo chini ya Kocha Mkuu, Mecky Maxime huku akitoa program kwa wachezaji wake.
Kwa Tanzania Ligi Kuu Tanzania Bara ilisimamishwa na Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Machi 17 ili kupisha zaidi maambukizi ya Virusi vya Corona.
Wakati ligi ikisimamishwa, Kagera Sugar ilikuwa nafasi ya nane na pointi zake kibindoni 41 huku ikiwa imecheza mechi 29 ambazo ni dakika 2,610.
Safu ya ushambuliaji iliyo chini ya Yusuph Mhilu mwenye mabao 11 ilitupia mabao 36 ina wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 72 huku safu ya ulinzi iliyo chini ya Juma Nyoso ikiruhusu mabao 31 ikifungwa bao moja kila baada ya dakika 84.
Kocha Mkuu, Maxime ili kujua mipango yake kwa sasa pamoja na program ambazo amewapa wachezaji wake huyu hapa anafunguka:-
“Ni kipindi kigumu ambacho tunapitia kwa sasa kwani hili janga ni la dunia nzima kiujumla sio upande mmoja kila mmoja anapambana kubaki salama.
Kipi ambacho kinafanyika kwa sasa?
“Kwetu sisi hakuna kinachoendelea kwani kambi tumevunja na sasa kila mchezaji yupo nyumbani akiendelea kuchukua tahadhari na kujilinda na Virusi vya Corona.
Kuna program ambazo wachezaji umewapa?
“Hilo lipo kwani kwa mchezaji kitu cha msingi ni kufanya mazoezi ili kuwa bora, maisha yao yanategemea mpira na ubora wao uwanjani ni lazima wafanya mazoezi.
“Kila mchezaji nimempa program yake ambayo anaifanya yeye binafsi akiwa nyumbani na familia yake.
Namna gani unawafuatilia wachezaji wako?
“Watu wazima ukiwapa kazi inakuwa ngumu kuwafuatilia ila nina amini kazi wanaifanya kwa wakati kwani dunia ya sasa imekuwa wazi sana kutokana na kukua kwa teknolojia.
“Kuna ule wakati ambao tunawafuatilia kupitia mitandao lakini sio kwa kiasi kikubwa kwani kikubwa ambacho wanatakiwa kukifanya kwa sasa ni kuchukua tahadhari wakiwa nyumbani.
Kipi ambacho kinakosekana kwa sasa?
“Kutokuwa pamoja kwa muda mrefu tulikuwa ni familia na tulizoea kuwa pamoja kwenye maisha yetu ya soka, ile burudani ambayo tulikuwa tunaitoa kwa mashabiki haipo kwa sasa tunaikosa.
Unadhani ligi ikirejea hali ya kikosi itakuaje?
“Mchezaji anatambua majukumu yake haijalishi itakuwa ni wakati gani ila kikubwa ni kusubiri mambo yatakuaje na hali itakuwa namna gani. Kikubwa ambacho ninaamini ni kwamba ligi itakaporudi nasi tutarudi uwanjani kuendelea kutoa burudani.
Tahadhari gani ambazo mnachukua kwa sasa?
“Hilo ni muhimu kwa kila mmoja na ni jambo la lazima kwani wanaopuuzia inabidi watambue Virusi vipo na tahadhari ni muhimu. Kwanza ni kufuata utaratibu ambao umewekwa na Serikali ili kila mmoja kuwa salama.
“Kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwani huwezi kujua hali inakuaje na nani yupo salama, muhimu kwa kila mmoja kutambua hili kwamba tahadhari ni jambo la msingi.
Ubora wa Kagera Sugar ulikuwa unabebwa na nini?
“Umakini wa wachezaji wangu kufuata maelekezo na kufanya yale ambayo ninawaelekeza ndani ya uwanja. Kila mmoja kutambua jukumu lake na kulifanya ilikuwa ni wakati mzuri ambao tulikuwa nao ila kwa sasa tunapambana na Virusi vya Corona,” anamalizia Maxime.
SOMA NA HII  RAIS WA TFF, WALLACE KARIA AWATAJA WACHEZAJI ANAOWAKUBALI, LUIS NA NIYONZIMA NDANI